MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba SC, Crescentius Magori amesema klabu hiyo imefikia hatua ya mwisho ya mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji uliodumu kwa miaka minane tangu ulipoanza mwaka 2017.

Magori aliyasema hayo jana kwenye mkutano na wanahabari kuelezea mchakato ya kusajili wanachama wapya wa klabu hiyo, huku akikiri mchakato huo ulikuwa mgumu kutokana na mfumo mpya wa uendeshaji unaotaka kuanzishwa, akieleza kuwa ni mfumo unaotumika zaidi katika nchi kama Ujerumani, lakini haukuwa umezoeleka Afrika.

Alifafanua, mfumo huo unagawanya umiliki wa klabu kati ya wanachama na wawekezaji, hali iliyosababisha changamoto kubwa za kisheria na kiutawala katika hatua za awali.

“Kusema ukweli, ni miaka minane iliyokuwa na changamoto nyingi sana, tulipitia juu na chini. Kuna wakati tulianza mchakato lakini tukakwama kwa sababu hatukupita sehemu fulani, tukapigwa faini na kulazimika kulipa,” amesema Magori.

Aliongeza katika safari hiyo, Simba ililazimika kupitia taasisi mbalimbali ikiwamo RITA, BMT hadi kufika Ofisi ya Waziri Mkuu kabla ya suala hilo kufikishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Magori amesema baada ya kukutana kwa vyombo vyote husika na kupitia changamoto zilizokuwapo, ushauri ulitolewa Simba na BMT wakae pamoja kumaliza tofauti zote, hatua iliyofungua mlango wa mafanikio ya sasa.

Hatua ya mwisho, Magori amesema ilikuwa ni wanachama kupitisha Katiba mpya ya klabu, ambayo alieleza kuwa ipo katika hatua za mwisho za kusajiliwa rasmi.

“Katiba hii kama si leo basi kesho au keshokutwa itasajiliwa. Hili ni jambo kubwa sana kwa Simba, maana sasa ndipo safari mpya inaanza rasmi,” amesema.

Kwa mujibu wa Magori, baada ya kukamilika kwa mchakato huo ndipo majukumu na mipango ya mwekezaji yataanza kuonekana wazi, ikiwamo kuwekeza katika miundombinu ya klabu.

Alibainisha kuwa moja ya maamuzi yaliyofanyika awali ilikuwa ni kusitisha utoaji wa kadi za wanachama, lakini sasa klabu iko tayari kurejesha zoezi hilo kwa nguvu mpya.

“Tunaenda kutoa kadi za wanachama na nina uhakika Simba itakuwa klabu ya kwanza kuwa na wanachama wengi, si Tanzania tu,” amesema.

Magori alieleza kuwa wanachama hao watakuwa si wanachama wa kawaida bali wanahisa wa klabu, jambo litakalowapa sauti na nafasi ya kushiriki katika maamuzi muhimu.

Aliongeza kuwa klabu inaandaa kadi za kisasa zitakazokuwa na faida mbalimbali kwa wanachama, ikiwa ni sehemu ya kuongeza thamani na ushiriki wao ndani ya Simba.

Katika hatua nyingine, Magori alieleza kuwa Simba ina bahati ya kuwa na mwekezaji ambaye ni mwanachama wa klabu hiyo, tofauti na baadhi ya klabu ambazo wawekezaji wao hutoka nje ya utamaduni wa timu husika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *