MAKUMBUSHO ya Dk Rashidi Mfaume Kawawa ni makumbusho yanayoelezea hali halisi ya maisha yake, maisha ya kawaida na maisha ya kiuongozi. Kiuongozi yanaelezea nyadhifa mbalimbali alizokuwa amezishika katika serikali ya Tanzania ikiwemo ya Waziri Mkuu na Makamu wa pili wa Rais.
Serikali imeifanya nyumba yake iliyojengwa mwaka 1974, Bombambili, Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kuwa Makumbusho ya inayobeba historia yake. Familia ya Dk Kawawa ilikabidhi nyumba hiyo Februari 27, 2016 kwa Makumbusho ya Taifa na kufunguliwa rasmi Februari 27, 2017 wakati wa Tamasha la Kumbukumbu ya Vita vya Majimaji.
Makumbusho hayo pamoja na mambo mengine yamehifadhi vitu mbalimbali yakiwemo mavazi, picha, tuzo na vitendea kazi alivyowahi kuvitumia ukiwemo mtambo wa kuoneshea sinema. Katika uhai wake, Dk Kawawa pia alipenda sanaa hasa uigizaji na moja ya filamu alizoigiza ni ile iliyojipatia umaarufu mkubwa iliyopewa jina la Mhogo Mchungu.
Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Dk Rashidi Kawawa, James Mfikwa anasema kwa kutambua umuhimu wake, serikali imeamua kuenzi kumbukumbu za maisha ya Dk Kawawa kwenye makumbusho hayo. Anasema moja ya maeneo muhimu waliyoona wayachukulie kwa uzito ni kuenzi mchango wake mkubwa kwenye sanaa ya filamu katika kukuza uzalendo, filamu alizoigiza kuanzia mwaka 1951 hadi 1954.
Mfikwa anamwelezea Dk Kawawa kuwa ndiye mwigizaji wa kwanza wa Kiafrika kucheza sinema tano kuanzia katika kipindi hicho. Anaitaja filamu ya ‘Mhogo Mchungu’ kama filamu ya kwanza kuigizwa na Kawawa mwaka 1951 ikifuatiwa na ‘Meli Inakwenda’ ambayo aliigiza mwaka 1952 na nyingine aliyoigiza mwaka 1953 ikijulikana kwa jina la ‘Wageni Wema.’
Kwa mujibu wa Mfikwa, filamu nyingine ni ‘Charo Amerudi’ na ‘Juma Matatani’ alizoziigiza mwaka 1954. “Katika kuenzi kazi za sanaa ambazo alikuwa akijihusisha nazo tumeona tuwe na jambo ambalo litakuwa linaendelea kukumbusha maisha yake hasa kwa upande wa Sanaa,” anasema.
Anaongeza, “Tumefikiria kuwa na onesho la sinema ambalo tutakuwa tunaonesha hizo sinema endapo tutazipata na kama zitapatikana …tutakuwa tunazionesha kwa awamu.” Anasema Makumbusho ya Dk Kawawa yatakuwa yakionesha sinema nyingine ambazo zina mrengo huo wa kimaadili ya Kitanzania na utakwenda sambamba na alizoigiza yeye.
Mfikwa anasema umuhimu wa kuenzi waasisi kwa waliyoyafanya ni kukuza yale mazuri na mema tukitolea mfano Dk Kawawa ambaye alijihusisha na sanaa ya filamu. Anasema Makumbusho yanahitaji kupita katika njia hiyo ili kukuza vipaji kwenye jamii ya Watanzania hasa uigizaji. “Dk Kawawa amejihusisha na sanaa ya uingizaji na hata michezo… Tutakuwa na programu za namna hii angalau kuenzi yale maisha ya Dk Kawawa ambayo aliyaishi,” anasema Mfikwa.
Mfikwa anasema viongozi wa Makumbusho ya Taifa wanaendelea kuzifuatilia filamu hizo pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kuoneshea filamu za Dk Kawawa. “Tunategemea kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2026; haya mambo yanaweza yakawa tayari na jamii itaanza kunufaika kwa kujifunza kuhusiana na maisha ya wazee wetu waasisi wa taifa, hasa Dk Kawawa,”
Kwa mujibu wa Mfikwa, majina ya filamu alizocheza Dk Kawawa ni ya kawaida yanayolenga kufundisha jamii ili iweze kueleza alichokusudia na kuwawezesha kujifunza, kuendeleza utamaduni wa Mtanzania na kukuza lugha ya Kiswahili.
Anasema kwa kutambua mchango wake katika tasnia ya Sanaa, uongozi wa Tamasha la Filamu la kila mwaka la Zanzibar (Zanzibar International Film Festival) kwenye onesho lake la Julai 11 hadi 18, mwaka 1998 lilimpatia tuzo Dk Kawawa ili kuenzi mchango wake kama gwiji wa utengenezaji wa filamu.
Pia, alipenda burudani hususani muziki hasa wa kikundi cha bendi ya TOT Plus inayomilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM), na ilimpatia tuzo ya heshima alipokuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa albamu ya tatu ya bendi ya TOT Plus.
Anasema lengo ni kuenzi mchango wake katika mwendelezo wa Bendi hiyo na alikabidhiwa akiwa Mwanachama na mpenda burudani wa kundi la TOT Plus. Pia, anasema Dk Kawawa alikuwa ni mpenda michezo na zaidi alikuwa ni mwamuzi wa mpira wa miguu na alijulikana ni mpenzi kubwa wa mpira wa miguu, nafasi ya mlinda mlango kwa maana ya golikipa.
Anasema kwa kutambua mchango wake katika sanaa, waandaji wa Tamasha la Kimataifa la Filamu Zanzibar (ZIFF) mwaka 1998 lilimpatia Dk Kawawa tuzo ili kuenzi mchango wake kama gwiji katika utengenezaji wa filamu. Mbali na mapenzi yake katika sanaa mbalimbali, Mfikwa anasema Dk Kawawa pia alikuwa mchezaji maarufu wa mchezo wa bao.
Anasema Kawawa alicheza wakati huo na viongozi wengi ikiwa ni njia mojawapo ya kuendeleza michezo ya jadi na ya kiutamaduni kwa Mtanzania. Mfikwa pia anakumbusha mchango mkubwa wa Dk Kawawa katika uanzishwaji wa vijiji vya ujamaa alipotekeleza maagizo ya Mwalimu Julius Nyerere.
Anasema ndani ya Makumbusho yake, kuna tuzo aliyotunukiwa kwa kutambua mchango wake katika jambo hilo. Historia inabainisha kuwa, Dk Kawawa alizaliwa Februari 27, 1926 katika Kijiji cha Matepwende, Tarafa ya Ligera wilayani Namtumbo katika Mkoa wa Ruvuma.
“Katika harakati zake za maisha,” historia inasema Kawawa alijenga nyumba hiyo na kuishi kwa kipindi kirefu cha maisha yake. Mmoja wa Wanaukoo wa Dk Kawawa, Shaibu Kaugo anamtaja Kawawa kama miongoini kwa viongozi wazalendo walioshiriki kupigania uhuru wa Tanganyika hadi kuzaliwa kwa Tanzania.
Kwa mujibu wa Kaugo, ni vigumu kwa Mtanzania kuzungumzia upatikanaji wa uhuru pasipo kulitaja jina la Kawawa. “Mzee Kawawa ameshika nyadhifa mbalimbai ukiwemo Uwaziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais; alikuwa mkali na hakupenda kusikia jina lake linatumiwa vibaya na watu wakiwemo wanafamilia ili kujipatia misaada,” anasema Kaugo. Anasema Kawawa hakusita kumuweka mahabusu mtu yeyote anayevunja sheria bila kujali ni mwanafamilia, au la hasa alipobaini mtu huyo anataka kuchafua jina lake.
Hata hivyo, anasema Kawawa alikuwa ni mtu mwenye huruma, utu na uaminifu hasa kwa taifa lake na alikuwa akipenda kusaidia maskini. SOMA: Ujenzi Makumbusho ya Mwalimu Nyerere Dodoma safi!
