KAULI ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka, aliyotoa wakati wa kikaokazi cha kitaifa cha Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais na maofisa habari wa serikali kilichofanyika Dar es Salaam, ni mwongozo muhimu unaopaswa kutekelezwa kwa vitendo.
Rai yake kwa maofisa habari kutumia taaluma yao kutoa taarifa sahihi, kwa wakati na kuzuia upotoshaji dhidi ya serikali, inaakisi uzito wa dhima waliyo nayo katika kulinda maslahi ya taifa. Ni bayana, katika mazingira ya sasa ya maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, taarifa husambaa kwa kasi kubwa. Ukimya wa maofisa habari pale serikali inapotupiwa lawama au upotoshaji, hutoa nafasi kwa taarifa potofu kukua, kuaminika na hatimaye kuichafua serikali pamoja na nchi kwa ujumla.
Ni katika muktadha huu, maofisa habari wanapaswa kutambua kuwa wao ndio wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutuliza hali, kuelimisha umma na kusafisha taswira ya taifa. SOMA: Maofisa habari watakiwa kuhamasisha amani EAC
Kama alivyosema katibu mkuu, ni wajibu wa maofisa habari kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huduma zinazotolewa na taasisi zao pamoja na changamoto zinazojitokeza. Wanapaswa kuwa tayari kutoa ufafanuzi wa haraka na sahihi pindi maswali, sintofahamu au upotoshaji unapojitokeza.
Taarifa za ukweli, zinapotolewa kwa wakati, zina uwezo wa kuzima moto kabla haujaleta madhara makubwa kwa maana ya imani ya wananchi kwa serikali yao kupotea. Tunaunga mkono msisitizo wa Katibu Mkuu Kiongozi kwamba maofisa habari wajikite kutangaza kazi na huduma za taasisi badala ya kusifia viongozi.
Balozi Kusiluka ameweka wazi kwamba taasisi ni kubwa kuliko mtu mmoja, na mafanikio ya serikali hupimwa kwa matokeo ya kazi zake kwa wananchi. Wananchi wanapopata taarifa sahihi kuhusu miradi, huduma na sera, hujenga uelewa, imani na ushirikiano na serikali.
Aidha, tunahimiza wakuu na watendaji wa taasisi za serikali kushirikiana bega kwa bega na maofisa habari. Ushirikiano huo utawawezesha maofisa hao kupata taarifa sahihi, za kina na kwa wakati, hivyo kuepusha kutoa majibu yanayochanganya umma au kuacha maswali bila majibu.
Msingi wa taarifa sahihi hujengwa ndani ya taasisi husika kupitia uwazi na ushirikishwaji. Ikumbukwe kuwa jamii inapokosa taarifa na majawabu ya masuala yanayoigusa, huwa rahisi kutunga simulizi mbadala, ambazo mara nyingi huwa za upotoshaji.
Upotoshaji huo unaweza kuaminika haraka na kuharibu taswira ya serikali na nchi. Ndiyo maana maofisa habari wanapaswa kuikinga nchi isichafuke kwa kutoa taarifa sahihi, na hata pale inapochafuka, wawahi kuisafisha kupitia mawasiliano ya ukweli, yenye weledi na uzalendo. Tunatambua rai kama hii imewahi kutolewa na pia wapo maofisa habari wanaofanya vizuri katika maeneo yao.
Hata hivyo, tunazidi kuwakumbusha maofisa hawa wasichukulie mazoea maagizo haya kutoka kwa viongozi wa juu. Wakitekeleza kwa vitendo rai ya Katibu Mkuu Kiongozi na wengine, maofisa habari watakuwa wametimiza wajibu wao wa kitaaluma na kizalendo wa kuisemea serikali, kuelimisha umma na kulinda heshima ya taifa.
