
Unguja. Wakati Serikali ikizipatia ufumbuzi kero 22 kati ya 25 za Muungano, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Hamad Yussuf Masauni amesema wizara hiyo itazitatua kero tatu za Muungano zilizobakia huku ikiangazia fursa mpya.
Amesema, wizara hiyo hahiitaji tena kuzungumza kuhusu changamoto za Muungano badala yake inahitaji kuzungumzia fursa zinazopatikana ndani ya Muungano huo.
Waziri Masauni amesema hayo leo Ijumaa Desemba 19, 2025 kwenye semina kuhusu Muungano kwa wahariri wa vyombo vya habari wa Zanzibar, iliyofanyika Maisara Mjini Unguja.
“Wizara hii inahitaji kuzungumza fursa zinazopatikana ndani ya Muungano badala ya kuzungumzia kero, mwelekeo wa wizara ni kuzitatua kero tatu zilizobaki zinazohusu Muungano,” amesema Masauni.
Hata hivyo, amesema mafanikio yaliyofikiwa katika miaka 61 ya Muungano hayapaswi kubezwa kwani zipo faida nyingi ambazo zinaonekana wazi na zile zisizoonekana moja kwa moja zinazoufanya Muungano huo uendelee kuimarika na kushamiri.
Amezitaja baadhi ya faida hizo kuwa ni kuimarika kwa udugu wa damu miongoni mwa wananchi, umoja na mshikamano wa kitaifa, kuimarika kwa ulinzi na usalama, kukua na kuimarika kwa biashara na fursa ya kutumia rasilimali zilizopo kwa pamoja.
Hivyo, amesema lazima kuendelea kuhakikisha muungano unakuwa imara zaidi kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho akisema msingi wa amani na utulivu wa Taifa ni Muungano wa Tanzania ambao umedumu zaidi ya miaka 6.
Amefafanua kuwa, matumaini ya Serikali, semina hii itakuwa na matokeo chanya katika kukuza uelewa kuhusu Muungano kwa kuendelea kuuenzi na kuudumisha kwa kuzingatia kuwa sekta ya habari ina wajibu wa kulinda na kuimarisha kupitia habari sahihi zinatolewa.
Vilevile, amesema vyombo vya habari vinawajibu wa kuzingatia maadili, sheria na taratibu ziliwekwa na nchi, hivyo amewasihi kuzingatia na kuheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatoa haki na wajibu ili kuepuka upotoshaji na uchochezi ambao unaweza kuondoa amani.
Masauni amewahakikishia wahariri na wananchi kuwa Serikali itaendelea kuheshimu na kukuza uhuru wa vyombo vya habari kama ilivyoelekeza Katiba na sheria zilizopo.
Mwanasiasa mkongwe Dk Harrison Mwakyembe amesema yapo majaribio mengi yaliyofanyika ila waasisi wa Muungano huo walisimama vizuri kuulinda.
Dk Mwakyembe ambaye amewahi kuwa waziri katika Serikali ya Muungano kwa miaka kadhaa amesema, viongozi hao waliamini kuwa nguvu ya Afrika ni ya pamoja na sio mtu mmoja mmoja ndio maana walianzisha njia za kujitegemea.
Amesema kipimo cha faida za Muungano ni hatua za maendeleo zilizopigwa visiwani humo akisema kuna mafanikio na hatua kubwa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Zanzibar, Hamza Hassan Juma amewataka wahariri kutumia vizuri nafasi zao kwa kuelimisha jamii kwani wengi wamezaliwa baada ya Muungano.
Amesema kwa sasa vyombo vya habari ndivyo vinavyotawala dunia na zipo changamoto zinazoukabili Muungano lakini busara za viongozi ndizo zinazodumisha Muungano huo.