Takwimu za hivi karibuni zaidi za vitendo vya uhalifu nchini Afrika Kusini zinaonesha kuwa zaidi ya watu 1,000 waliuawa katika Mkoa wa Western Cape kati ya mwezi Julai na Septemba mwaka huu, huku Cape Town ikiwa kitovu cha vitendo vya uhalifu na vurugu katika eneo hil.

Kamishna wa Polisi wa Western Cape, Thembisile Patekile, ametoa takwimu mpya za vitendo vya uhalifu ndani ya mkoa huo na kusema kuwa, kesi 1,160 za mauaji zilirekodiwa katika jimbo hilo kwenye kipindi cha baina ya miezi hiyo ikiwa ni ongezeko la asilimia 9.1 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana. Majaribio ya mauaji pia yaliongezeka kwa asilimia 4.8 na kufikia hadi kesi 1,157 katika kipindi hicho.

Kwenye robo ya tatu ya mwaka huu, Jiji la Cape Town limesharekodi  kesi 967 za mauaji, likiwa ni ongezeko la asilimia 8.9 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.

Thembisile Patekile amesema kuwa ongezeko hilo la vitendo vya uhalifu linatokana na kuongezeka vurugu za magenge, uporaji katika usafiri wa teksi, ugomvi wa maneno, mashambulizi ya kulipiza kisasi, unyang’anyi na vurugu za kijinsia.

Silaha za moto zimeendelea kuwa ndizo silaha zinazotumika zaidi katika vitendo hivyo vya uhalifu. Zimetumika kwa asilimia 60.6 kwenye kesi zote za mauaji huko Afrika Kusini. 

Kwa mujibu wa takwimu mbalimbali, operesheni za jeshi la polisi zilizofanyika katika robo mbili za kwanza za mwaka huu zilipelekea kukamatwa silaha 1,291 na risasi 32,476 za aina mbalimbali. Polisi pia walikamata silaha hatari 12,924 na kuwatia mbaroni watu 137,081 katika kipindi hicho.

Vilevile kwenye kipindi hicho hicho, wanachama 114 wa magenge ya wahalifu, wakiwemo viongozi wanane wa magenge hayo, walikamatwa, huku washukiwa 65 wakishikiliwa kwa makosa yanayohusiana na utekaji nyara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *