Miradi ya kimkakati kuleta neema ya ajiraMiradi ya kimkakati kuleta neema ya ajira

SERIKALI ya Awamu ya Sita inatarajia kufufua miradi ya kimkakati iliyokwama kwa muda mrefu, ikiwemo miradi ya chuma na makaa ya mawe ya Mchuchuma na Liganga.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Biashara na Viwanda Judith Kapinga amesema kuwa mradi wa chuma unatarajiwa kuzalisha ajira 1,000. “Mradi huu ulikwama kwa muda mrefu lakini Rais Samia Suluhu Hassan ametuwekea mazingira mazuri na sasa majadiliano yanaendelea ili kuhakikisha tunapiga hatua na mradi huu unatekelezwa,” alisema Kapinga.

Ameongeza kuwa, katika mradi huo vijana wenye ujuzi wa ufundi, uhandisi, uchimbaji, usambazaji na biashara watapata nafasi kubwa za ajira. “Aidha, kwa sasa serikali ipo katika hatua nzuri ya majadiliano na mwekezaji ili kuanza utekelezaji wa mradi na tayari serikali imelipa fidia zote kwa wananchi waliopisha eneola mradi,” alisema.

Kapinga amesema  mradi wa uchimbaji chuma una akiba kati ya tani milioni 700 hadi bilioni 1.4, huku uzalishaji wa chuma ukitarajiwa kufikia tani milioni 2.9 kwa mwaka. Amesema uchimbaji wa chuma utafanyika kwa kipindi cha miaka 50, huku kwa upande wa makaa ya mawe kukiwa na akiba ya tani milioni 428 na uzalishaji wa tani milioni tatu kwa mwaka, kwa muda wa miaka 142.

Pia, Kapinga ameeleza  nia ya serikali ya kukwamua mradi wa uchimbaji wa magadi soda wa Engaruka wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 700. Mradi huo unatarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja kati ya 1,000 hadi 1,400 na ajira zisizo za moja kwa moja 4,000 hadi 5,600. “Tanzania itakuwa mzalishaji namba moja wa magadi soda barani Afrika,” alisema.

Ametaja mradi mwingine kuwa ni wa chuma wa Maganga Matitu wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 77.45, unaotarajiwa kuzalisha chuma kwa kiwango kikubwa na kutoa ajira 1,000 utakapokamilika. Amesema miradi hiyo ni fursa kwa vijana kupata ajira na kuanzisha biashara zitakazotoa huduma mbalimbali, huku mradi wa makaa ya mawe wa Katewaka ukitarajiwa kuzalisha tani milioni 1.5 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka 100.

Kadhalika, Kapinga amesema serikali inaendelea kufanya mapitio ya biashara zinazopaswa kufanywa na wazawa, kama jitihada za kuthamini ujasiriamali wa wazawa na kuongeza ajira kwa Watanzania. Amesema serikali inaweka mipaka ili kuhakikisha wazawa wanapata nafasi ya kuendeleza biashara zao, hatua itakayolinda ajira, kukuza vipaji vya vijana na kuimarisha uchumi wa ndani, licha ya changamoto ya baadhi ya wazawa kusajili biashara kwa kivuli cha wageni.

“Tunafanya mapitio mwezi huu kuona mapungufu na namna ambayo tutaboresha lakini tutaweka udhibiti kwa wale wanaofungua kampuni na kumuweka mgeni, kwa sababu tulishakubaliana tutalinda biashara za wazawa,” alisema. SOMA: Jafo ataka mradi makaa ya mawe ukamilike haraka

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *