Kauli ya Museveni imekosolewa na mpinzani wake mkuu Robert Kyagulanyi ambaye amewatahadharisha polisi na wanajeshi kutokubali kuwaua wananchi wenzao wakilinda maslahi ya kiongozi asiyeheshimu maisha ya binadamu. Matamshi ya rais Yoweri Museveni yameibua maoni kwamba vitisho vyake vyaweza kusababisha raia wengi wasijitokeze kupiga kura.
Mwanahabari mmoja kwenye mojawapo ya vikao vya jioni baada ya kufanya kampeni alimtaka rais Museveni atoe kauli yake kuhusu mwito wa kila mara wa mpinzani wake Robert Kyagulanyi kuwataka wapigaji kura kubaki kwenye vituo kuhakikisha kura zao haziibiwi. Rais Museveni ambaye ni mgombea kwa tiketi ya chama tawala NRM alisema:
” Nimekuwa nikimsikia Kyagulanyi akisema askari ni wachache na wanaoweza kufanya vurugu ni wengi. Msimsikilize kwa sababu kila askari ana risasi 120 na mkisema wanaofanya vurugu ni wengi, walingenisheni na idadi ya risasi za askari.”
Tamko hilo limeibua maoni ya hisia za hofu na wasiwasi miongoni mwa wananchi wengi. Wakielezea kuwa amani na uthabiti havidumishwi tu kwa njia ya kutumia bunduki. Baadhi wamesema:
” Huahidi amani kwa watu kwa kuwambia una risasi na bunduki. Hapajawahi kutokea vita duniani ambapo watu wengi wanaopinga jambo fulani kwa pamoja hushindwa kupitia kwa bunduki.”
Ukosoaji kutoka kwa mpinzani mkuu
Kwa upande wake mgombea wa chama kikuu cha upinzani NUP Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine amemshtumu vikali rais Museveni kwa tamko hilo akiwashauri polisi na wanajeshi wasikubali kutumiwa kuwaua wananchi wenzao ambao wanatekeleza haki zao kisheria wanaposhiriki na kuhakikisha kuwa kura zao haziibiwi.
” Ujumbe wangu kwa polisi na wanajeshi: Huyu bwana amezeeka na anaondoka na nyinyi mnajua kwa mujibu wa sheria za haki za binadamu binafsi mtawajibikia vitendo vyoyote vinavyokiuka haki za binadamu. Watu ambao Museveni anawambia kuwaua ni ndugu, dada, jamaa na wananchi wenzenu,” alisisitiza Bobi Wine.
Kwa sasa suala hilo la wapigaji kura kubaki kwenye vituo kusubiri matokeo limeibua mjadala mkubwa ndani nan je ya bunge la Uganda . Mjadala huo uliibuka pale mkuu wa majeshi Jenerali Muhoozi Kainerugaba ambaye pia ni mwanawe rais Museveni alipotoa onyo hilo. Hata wiki hii kwenye sherehe za kuvisha maafisa wa jeshi chepe, jenerali huyo alirudia tamko hilo kwa kusema:
” Tunatoa mwito kwa wananchi kupiga kura kwa amani na waende nyumbani. Wasibaki kwenye vituo vya kupigia kura. Watakaojaribu kuzusha vurugu tutachuwakulia hatua za haraka kwa kutumia zana zozote tulizo nazo.”
Uchaguzi mkuu nchini Uganda utafanyika tarehe 15 mwezi Januari mwakani. Kwa sasa wagombea 8 wa urais wanasaka kura sehemu mbalimbali za nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
