IRINGA: Mradi wa NBS–USANGU umeendesha mafunzo ya siku tano kwa Kamati za Kushughulikia Malalamiko za Vijiji katika maeneo ya utekelezaji wa mradi huo, kwa lengo la kuimarisha haki, uwazi na ufanisi katika kushughulikia changamoto za wananchi.

Mafunzo hayo yamefanyika Rujewa, wilayani Mbarali, kuanzia Desemba 15 hadi 20, yakihusisha wajumbe kutoka vijiji vinavyonufaika na mradi.

Mradi wa NBS–USANGU (Nature-Based Solutions – Usangu) unalenga kulinda na kurejesha mazingira ya Bonde la Usangu, kuboresha  usimamizi wa rasilimali za maji, kukuza kilimo rafiki kwa mazingira, na kuimarisha ustawi wa jamii kwa kushirikisha wananchi kikamilifu katika maamuzi na utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mratibu wa Mradi wa NBS–USANGU, David Muginya, alisema uwepo wa mifumo madhubuti ya kushughulikia malalamiko ni nguzo muhimu ya mafanikio ya mradi na ulinzi wa haki za wananchi.

“Tunataka jamii iwe na imani na mradi huu. Malalamiko yakishughulikiwa kwa haki na kwa wakati, migogoro inapungua na ushiriki wa wananchi unaongezeka,” alisema Muginya.

Alisisitiza kuwa mradi huo unaamini katika ushirikishwaji wa jamii kama msingi wa maendeleo endelevu na amani ya kijamii.

Mafunzo hayo yaliendeshwa na Legal Services Facility (LSF), ambapo wataalamu waliwasilisha mada kuhusu mifumo ya kushughulikia malalamiko, haki za jamii, uwajibikaji na ufuatiliaji wa utekelezaji wa maamuzi.

Said Chitungi, Menaja Ufuatiliaji na Matokeo wa LSF, alisema kamati za malalamiko zina jukumu la kipekee la kuwa daraja kati ya wananchi na miradi ya maendeleo.

“Kamati hizi zikifanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia ushahidi, zinaweza kuzuia migogoro na kulinda haki za wananchi,” alisema.

Kwa upande wake, Victoria Mshana, Afisa Mradi wa LSF, alisema mafunzo hayo yamezingatia masuala ya jinsia, usawa na ujumuishaji wa makundi maalum ili kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma.

Washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kuridhishwa na maudhui yaliyotolewa huku Ramadhani Silapola akisema mafunzo hayo yamewapa mwongozo wa kitaaluma wa kutekeleza majukumu yao kwa haki na uwazi.

Naye Rachel Mgalla alisema elimu waliyoipata itasaidia kujenga uhusiano mzuri kati ya jamii na mradi wa NBS–USANGU.

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za mradi kuhakikisha utekelezaji wake katika Bonde la Usangu unazingatia misingi ya uwazi, uwajibikaji na maendeleo endelevu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *