Putin ameyasema hayo wakati wa mkutano wake wa mwisho wa mwaka na waandishi wa habari ambapo amewaambia Warusi kuwa Moscow inalenga kuzidisha shinikizo kwa Ukraine.
Putin mwenye umri wa miaka 73, amerudia mara kadhaa katika wiki za hivi karibuni kuwa Moscow itainyakua ardhi ya Ukraine, ambayo anadai ni ya Urusi, kwa nguvu iwapo mazungumzo yatafeli.
Kiongozi huyo wa Urusi vilevile amesema kuwa hahisi kuwa yeye binafsi amehusika na vifo vya makumi kwa maelfu ya watu waliofariki tangu kuanza kwa vita hivyo mwaka 2022.
Maeneo zaidi kuchukuliwa Ukraine kabla mwisho wa mwaka
Ameongeza kuwa hatua inazozidi kupiga Urusi nchini Ukraine katika siku za hivi majuzi zitaipelekea Ukraine kuingia katika makubaliano.
Akitaja miji kadhaa mashariki mwa Ukraine inayolengwa na jeshi la Urusi, Putin amesema ana uhakika kuwa Moscow itachukua maeneo zaidi kabla mwishoni mwa mwaka.
Wakati huo huo, Putin amesema kuwa Urusi haina nia ya kuishambulia Ulaya iwapo itapewa heshima yake. Ameyasema hayo huku kukiwa na hofu kwamba Moscow ni kitisho cha usalama wa mataifa ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO yaliyoko mashariki mwa Ulaya.
Amesema yuko tayari kwa mazungumzo ya amani yatakayoangazia chanzo cha msingi cha vita hivyo nchini Ukraine.
“Mimi pia ningependa kuona kuwa tunaishi kwa amani mwaka ujao, bila makabiliano yoyote ya kijeshi. Na narudia, tungependa sana, tunajitahidi kusuluhisha masuala yote yenye utata kwa njia ya mazungumzo. Na nafikiri mutakubaliana na hili pia. Tunastahili kuhakikisha kuwa vyanzo vikuu vya mzozo huu vinaondolewa, ili kusitokee kitu kama hiki katika siku zijazo, ili amani iwe ya kudumu. Hili ndilo tutakalolipigania,” alisema Putin.
Haya yanafanyika wakati ambapo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kuwa Ulaya italazimika kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Putin, endapo juhudi zinazoongozwa na Marekani za kusitisha vita vya Ukraine hazitozaa matunda.
Mkopo kwa Ukraine ni ishara vita vinastahili kuisha
Mataifa mengi ya Umoja wa Ulaya isipokuwa Hungary na Slovakia, yamekatisha mawasiliano na Putin tangu aivamie Ukraine. Na sasa Macron anasema Ulaya haitokuwa na budi ila kuwasiliana na kiongozi huyo wa Urusi.
Kwa upande wake Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ambaye yuko ziarani nchini Poland, amesema hatua ya Umoja wa Ulaya kuamua kuipa nchi yake mkopo wa yuro bilioni 90, ni ishara tosha kwa Urusi kwamba hakuna haja ya kuendelea na vita kwa kuwa Ukraine inafadhiliwa.
Zelenskiy amesisitiza kuwa uamuzi huo uliofikiwa huko Brussels ni ushindi kwa Ukraine kwani inakabiliwa na mapungufu ya yuro bilioni 45 katika bajeti yake ya mwakani, na kwamba inapanga kuzitumia fedha hizo za Umoja wa Ulaya katika masuala ya kijamii na kiutu na kusaidia pia katika juhudi zake za ulinzi.
Vyanzo: AFP/AP/Reuters