
Kiongozi huyo wa Marekani ameongeza kwamba kutakuwepo na ukamataji zaidi wa meli za mafuta karibu na pwani ya Venezuela. Marekani tayari iliikamata meli moja ya mafuta iliyokuwa chini ya vikwazo nje ya pwani ya Venezuela wiki iliyopita.
Mnamo siku ya Jumanne, Donald Trump aliagiza kuweka kizuizi dhidi ya meli zote za mafuta zinazoingia na kutoka Venezuela, ikiwa ni hatua ya hivi karibuni ya Washington kuongeza shinikizo kwa serikali ya Nicolas Maduro, kwa kulenga chanzo chake kikuu cha mapato.
Serikali ya Venezuela imejibu kwa kuitaja hatua hiyo kama uvamizi wa wazi wa mali yake.
Katika mahojiano hayo na NBC, Trump hata hivyo alikataa kuweka wazi iwapo nia yake kuu ni kumuondoa madarakani Rais Nicolas Maduro.