
Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, jana Alkhamisi alisaini sheria ambayo itapanua Bunge la nchi hiyo, hatua ambayo wakosoaji wanasema inaweza kukinufaisha chama chake, miezi minane kabla ya uchaguzi wa kitaifa.
Mabadiliko hayo yataongeza idadi ya wabunge hadi takriban 280 badala ya 167 waliopo sasa, kwa kuunda majimbo zaidi ya uchaguzi, kutenga viti vipya 40 kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, na kumruhusu rais kuteua wabunge 11 badala ya wanane kama ilivyokuwa hapo awali.
Wakosoaji, ikiwa ni pamoja na Kanisa Katoliki la Zambia, wanasema mabadiliko hayo yanaweza kukinufaisha chama cha Hichilema katika uchaguzi wa rais na wabunge uliopangwa kufanyika Agosti 2026.
Hichilema, ambaye atagombea muhula wa pili wa urais katika uchaguzi huo, amesema wakati wa sherehe ya utiaji saini sheria hiyo kwamba mabadiliko hayo yanafanywa kwa nia njema na kwamba mashauriano ya kutosha yamefanyika kabla ya kupasishwa.
Mwanaharakati wa haki za binadamu, Prebner Changala ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba “chama cha Hichilema kinaweza kutumia mabadiliko ya katiba kwa faida yake katika uchaguzi ujao,” akiongeza kwamba “hamu kuu ni kuimarisha madaraka kwa kuchora upya mipaka katika ngome za chama tawala.”
Baadhi ya wanasiasa wa upinzani nchini Zambia pia wamekosoa hatua ya kuongeza idadi ya wabunge wakati ambapo nchi bado inatoka katika mgogoro wa deni wa muda mrefu.