Viongozi hao lakini wameshindwa kukubaliana kutumia mali za Urusi zilizofungiwa ili kutoa ufadhili huo.

Makubaliano hayo yaliyofikiwa usiku wa manane katika mkutano wa kilele uliofanyika huko Brussels, Ubelgiji, unaipa Ukraine nguvu mpya ilizokuwa inazihitaji mno wakati ambapo Rais wa Marekani Donald Trump anashinikiza kupatikana kwa makubaliano ya haraka ya vita hivyo vya Ukraine na Urusi vilivyodumu kwa takriban miaka minne, kufikia mwisho.

Huku Ukraine ikiwa huenda imeshushwa mabega kidogo na hatua ya Umoja wa Ulaya kutofikia makubaliano ya kutumia mali za Urusi, kupatikana kwa ufadhili kwa njia nyengine pia ni ahueni.

Hakikisho la ufadhili kwa Ukraine kwa miaka ijayo

Hii ni kwa kuwa mwanzoni mwa mkutano huo wa kilele, Zelenskiy alikuwa amewaambia viongozi hao wa Ulaya kuwa kunahitajika uamuzi kufikia mwisho wa mwaka, na kwamba kuiweka nchi yake katika nafasi yenye nguvu, kutaipatia fursa nzuri kwenye mazungumzo ya kusitisha vita.

Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban
Waziri Mkuu wa Hungary Viktor OrbanPicha: Nicolas Tucat/AFP/Getty Images

Antonio Costa ni Rais wa Baraza la Ulaya.

“Tumekubaliana kuweka vikwazo dhidi ya Urusi. Lengo letu si kurefusha vita, isitoshe, maamuzi ya leo ni mchango muhimu katika kupatikana kwa amani ya haki na ya kudumu nchini Ukraine, kwasababu njia ya pekee ya kuileta Urusi kwenye meza ya mazungumzo ni kwa kuiimarisha Ukraine,” alisema Costa.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa X ameyasifu makubaliano hayo akisema ni muhimu kuwa nchi yake imepokea hakikisho la ufadhili kwa miaka ijayo.

Majadiliano kuhusu kuipa Ukraine mkopo kutokana na mali za Urusi yalikuwa magumu na wazo la ufadhili huo kupatikana kwa Ulaya kuomba mikopo, awali lilionekana kama lisilowezekana kwani linahitaji makubaliano ya pamoja, na Hungary ambayo Waziri Mkuu wake Viktor Orban ni mwandani wa Rais Vladimir Putin, ilikuwa imelipinga.

Ila Hungary pamoja na Slovakia na Jamhuri ya Czech baadae walikubali mpango huo wa mkopo usonge mbele, mradi tu usiwaathiri kifedha.

Kigingi kikuu kilikuwa kuipa Ubelgiji hakikisho la kutosha kuwa ikitoa fedha za Urusi kutumika basi itaungwa mkono na Ulaya kikamilifu dhidi ya hatari za kifedha na kisheria kutoka kwa Urusi. Ubelgiji ndiyo inayoshikilia yuro bilioni 185 ya mali za Urusi zenye thamani ya yuro bilioni 210 zilizofungiwa barani Ulaya.

Ukraine yahitaji yuro bilioni 135

Kama anavyoeleza Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, viongozi wa Ulaya wamesema kuwa mali hizo za Urusi zitaendelea kufungiwa, hadi pale Moscow itakapoifidia Ukraine kutokana na uharibifu uliosababishwa na vita vyake.

“Ulaya imeuelewa ujumbe, Ulaya imeonesha uhuru wake. Tunasimama dhidi ya kitisho kikubwa zaidi cha sera ya usalama Ulaya, ambacho ni uchokozi wa Urusi ambao umekwenda zaidi ya uchokozi kwa Ukraine. Ukraine sasa imehakikishiwa ufadhili kwa miaka kadhaa, kama nilivyoomba tayari Oktoba. Mtazamo huu ni muhimu kuhakikisha Ukraine haianguki ila pia kutuma ujumbe kwa Moscow,” alisema Merz.

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz
Kansela wa Ujerumani Friedrich MerzPicha: John Thys/AFP/Getty Images

Umoja wa Ulaya unakadiria kuwa Ukraine inahitaji yuro bilioni 135 zaidi ili iweze kujikimu katika miaka miwili ijayo, kwani mapungufu ya fedha yataanza kuikabili Aprili mwakani.

Urusi kwa upande wake kupitia afisa wake mkuu wa kiuchumi Kirill Dmitriev, imeonesha kuridhishwa na hatua ya Ulaya kutofikia makubaliano ya kutumia mali zake. Katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa Telegram, Dmitriev amesema, “kwa sasa, sheria na akili ya kuzaliwa vimeshinda.”

Vyanzo: AFP/Reuters/DPA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *