
Costa aliandika kupitia mtandao wa X akithibitisha juu ya uamuzi huo na kwamba fedha hizo zitatumia kwa mwaka 2026 hadi 2027.
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amesema mapema leo kwamba kwamba Umoja wa Ulaya umetuma “ishara ya wazi” kwa kiongozi wa Urusi Vladimir Putin kufuatia makubaliano hayo. Ameandika kupitia mtandao wa X kwamba, huo ni ujumbe kwa Putin kwamba, Vita vyake nchini Ukraine havitakuwa na maana tena.
Makubaliano hayo hata hivyo hayatakuwa na athari yoyote ya kifedha kwa Hungary, Slovakia na Jamhuri ya Czech, ambazo hazikutaka kuchangia katika ufadhili huo, taarifa zimesema na kuongeza kuwa serikali za Ulaya pamoja na Bunge la Ulaya wataendelea kushughulikia kuandaa mkopo kwa ajili ya Ukraine ambao utategemea mali za benki kuu ya Urusi zilizozuiliwa.
Viongozi hao wa Ulaya walilazimika kukaa hadi usiku wa manane kwa lengo la kutafuta makubaliano na kuihakikishia Ubelgiji kwamba wangetoa dhamana ya kuilinda ikiwa Urusi itataka kulipiza kisasi kufuatia hatua ya taifa hilo kuunga mkono mkopo huo.
Mazungumzo yaliangazia pia kuipa hakikisho la usalama Ubelgiji
Mazungumzo hayo pia yalijikita katika kuihakikishia Ubelgiji inayohifadhi kiasi kikubwa cha mali hizo, pamoja na mataifa mengine yanayoonyesha wasiwasi kwamba Ulaya huenda ikajikuta katika mizozo ya kisheria na kifedha.
Ubelgiji inahofia kwamba Urusi italipiza kisasi na inautaka umoja huo kukopa fedha hizo kwenye masoko ya kimataifa. Sehemu kubwa ya mali hizo za karibu yuro bilioni 193 zimehifadhiwa na taasisi ya fedha ya Ubelgiji ya Euroclear, yenye makao yake makuu Brussels.
Rasimu mpya ya makubaliano yaliyoandaliwa kwa ajili ya mazungumzo ya viongozi hao iliipa Ubelgiji na nchi nyingine dhamana isiyo na kikomo ikiwa Moscow itawashtaki. Ahadi kama hiyo inaambatana na masharti ya Ubelgiji, ingawa wanadiplomasia walitahadharisha kwamba huenda ingezisababishia matatizo baadhi ya serikali ambazo zingehitaji idhini ya bunge ili ahadi kama hiyo ipate kibali.
Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk alinukuliwa akisema wakati akiingia kwenye mazungumzo hayo kwamba, ni ama wanakubaliana ili kupata fedha hizo ama kuendelea kushuhudia damu ikimwagika, huku akiwatolea wito viongozi wa Ulaya kulikubali pendekezo hilo. Wengi wao aidha wanaiona Urusi kama kitisho cha kiusalama na wanataka kuendelea kuifadhili Ukraine ili iweze kuendelea kupambana.
Mara baada ya kufika Brussels, rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alikutana na Waziri Mkuu wa Ubelgiji ili kuwasilisha hoja yake kuhusu fedha hizo kutolewa. Nchi hiyo iliyokumbwa na vita iko hatarini kufilisika na inahitaji fedha nyingine ifikapo majira ya machipuko. Aliwaambia waandishi wa habari na hapa namnukuu “Ukraine ina haki ya kutumia fedha hizi kwa sababu Urusi inatuangamiza na kutumia mali hizi dhidi ya mashambulizi haya ni haki kabisa.”
Hungary na Slovakia zinapinga suala la mkopo wa fidia. Mbali na Ubelgiji, Bulgaria, Italia na Malta pia hazifanya maamuzi.