
Usafirishaji wa bidhaa kote duniani unatazamiwa kuwa wa gharama nafuu zaidi, unaofanyika kwa kasi zaidi na kwa urahisi mkubwa, kufuatia kupitishwa makubaliano mapya yanayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ambayo yanahuisha nyaraka zinazotumika katika usafirishaji wa kimataifa.
Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Hati za Mizigo Zinazoweza Kuhamishika,(United Nations Convention on Negotiable Cargo Documents, unaanzisha kwa mara ya kwanza, hati moja inayoweza kutumika kwa treni, malori na ndege, na kuruhusu mabadiliko ya kimkakati ya usafirishaji kufanywa kwa bidhaa ambazo tayari ziko safarini.
Anna Joubin-Bret, Katibu wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Sheria ya Biashara ya Kimataifa (UNCITRAL), iliyoongoza mazungumzo ya miaka mitatu amesema: βhili ni jambo la kubadili mchezo kabisa kwa biashara ya kimataifa. Ni hati moja ya usafiri iliyo ya aina nyingi (multimodal), ya kielektroniki kikamilifu, na inayoweza kuhamishika.β
Kwa sasa, hati za usafiri zinazoweza kuhamishika hutumika zaidi kwa bidhaa zinazosafiri kwa bahari, ambako safari zinaweza kuchukua wiki kadhaa. Bidhaa kama mafuta au kakao mara nyingi huuzwa mara kadhaa zikiwa baharini bei zinapobadilika.
Imeelezwa kuwa, mkataba huo utakuwa muhimu hasa kwa nchi zisizo na bandari na nchi zinazoendelea, kwa kuwasaidia kujiunganisha zaidi na mfumo wa biashara ya kimataifa na kupunguza gharama.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio linalounga mkono mkataba huo tarehe 15 Desemba 2025. Hafla ya kutia saini imepangwa kufanyika nusu ya pili ya mwaka 2026 mjini Accra, Ghana.
Mkataba huo utaanza kutekelezwa mara tu nchi kumi zitakapouridhia…/