
Ofisi ya Kamishna Mkuu wa shirika la kuhudumia wakimbizi la UNHCR imesema, baada ya mapigano ya hivi karibuni yaliyotokea Kivu Kusini, hususan katika mji wa Uvira, kumeshuhudiwa wimbi jipya la wakimbizi tangu Disemba 5, wanaokadiriwa kufikia 80,000 wanaokimbilia nchini Burundi.
Wakimbizi hao wanajumuisha Wakongomani 71,989 na Waburundi 8,000.
Shirika hilo ambalo linatarajia kupokea jumla ya wakimbizi wapya 90,000, limezindua kampeni ya msaada wa dola milioni 33 ili kuwahudumia wakimbizi na kuwapatia makaazi salama.
Meya wa mji wa Rumonge kusini-magharibi mwa Burundi, Augustin Minani, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hali ni mbaya mno katika mji huo ambapo wakimbizi kati ya 20,000 hadi 25,000 kutoka Kongo wamewasili na wanakosa mahitaji ya msingi ikiwemo chakula.