
Dar/Moro. Sintofahamu imeibuka kufuatia kifo cha binti wa kazi, Mwanahasan Hamis (18), aliyefariki dunia jijini Dar es Salaam na mwili wake kusafirishwa kwenda Mvomero, Morogoro kwa maziko, baada ya ndugu kudai umeondolewa viungo.
Kufuatia tukio hilo lililotokea jana Jumatano, Desemba 17, 2025, katika kijiji cha Lusanga, Wilaya ya Mvomero, magari mawili yaliyotumika kusafirisha mwili huo kutoka Dar es Salaam yalichomwa moto, taarifa ya Polisi Mkoa wa Morogoro imedhibitisha.
Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 18, 2025, mjomba wa marehemu, Yusuph Aheri, amesema walibaini upande wa kushoto na kulia wa mwili wa binti yao, kuanzia magotini hadi kwenye kitovu, kulifanyika upasuaji.
Amesema baada ya tukio hilo na uchunguzi kufanyika, wamepatiwa majibu ya vipimo vya uchunguzi yanayoeleza kuwa hakukuwa na tatizo lolote kwenye mwili wa binti yao, jambo ambalo hawakuliridhia, lakini wamekubali kuuzika mwili kwa kuwa hawana la kufanya.
“Ni kweli tumepewa taarifa, lakini majibu tuliyopewa ni kama daktari alifungua mwili na kuangalia kwa macho. Wanasema kilichofanyika ni kuweka dawa ili mwili usiharibike,” amesema.
Amesema baada ya kuhoji kwa nini upasuaji ufanyike kwa namna hiyo, hawakuridhika na majibu waliyopewa, lakini wamekubali kuuzika mwili kwa kuwa hawana nguvu ya kuchukua hatua zaidi.
Akizungumzia madai ya kuondolewa kwa viungo vya mwili, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, amesema hilo ni suala la kitaalamu ambalo daktari ndiye mwenye uwezo wa kulielezea.
“Baada ya taharuki kutokea, tuliwachukua waliouleta mwili na kuwapeleka hospitalini kwa wataalamu wa viungo vya binadamu. Huyu mtu aliugulia hospitalini na kulitolewa kibali cha mazishi,” amesema.
Kamanda Mkama amesema uchunguzi wa kisayansi tayari umefanyika na ndugu wa marehemu wamekabidhiwa ripoti.
Tukio lilivyokuwa
Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Lusanga, Turiani, mkoani Morogoro, Abdallah Kilimo, amesema alipata taarifa kuwa mwili wa binti aliyekwenda kufanya kazi Dar es Salaam umerejeshwa nyumbani baada ya kufariki dunia.
Amesema walioupeleka mwili nyumbani walieleza kuwa marehemu alisumbuliwa na malaria, ambayo ilidaiwa kuwa chanzo cha kifo chake.
“Taarifa nilizipata msikitini ni kwamba kutakuwa na swala ya adhuhuri kwa ajili ya marehemu na baadaye maziko. Baada ya swala, nikiwa njiani kwenda msibani, nilikutana na kina mama wakikimbia wakisema fujo zimetokea,” amesema.
Ameeleza alipofika eneo la tukio alimkuta mkuu wa Kituo cha Polisi Mtibwa.
“Nilipoona magari yamechomwa moto, nilimuuliza mkuu wa kituo kama alikuwa na taarifa na kama anahitaji msaada. Askari wengine walikuja wakiwa na silaha na mabomu ya machozi, taharuki ikaongezeka,” amesema.
Amesema polisi walianza kutuliza vurugu baada ya wananchi kudai kuwa mwili wa marehemu umeondolewa viungo.
Baada ya polisi kuwaomba wananchi waache fujo na kuruhusu uchunguzi kufanyika, hali ilitulia na wahusika kutoka kwenye familia pamoja na watuhumiwa walichukuliwa kwa ajili ya mahojiano.
“Wameenda kukagua na imeonekana hakuna chochote kilichofanyika. Mwili tunauzika leo,” amesema.
Taarifa ya Polisi
Katika taarifa yake, Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limesema linafanya uchunguzi kubaini chanzo cha kuchomwa moto na kuharibiwa kwa magari mawili katika Wilaya ya Mvomero.
Tukio hilo lilitokea katika kitongoji cha Kilingeni, kijiji cha Lusanga, kata ya Diongoa, tarafa ya Turiani, ambapo magari aina ya Mazda CX-5 na Toyota Noah yalichomwa moto, hali iliyohatarisha maisha ya watu waliokuwapo eneo hilo.
Inaelezwa magari hayo yalikuwa yakisafirisha mwili wa marehemu Mwanahasan Hamis, mfanyakazi wa kazi za ndani na mkazi wa Turiani, aliyefariki dunia na alikuwa akisafirishwa kwenda mkoani Morogoro kwa ajili ya shughuli za mazishi.
Taarifa zinaeleza kuwa wakati taratibu za mazishi zikiendelea, kulitokea taharuki miongoni mwa wananchi kutokana na mashaka kuhusu mazingira ya kifo cha marehemu.
Hali hiyo ilisababisha vurugu zilizochochea uchomaji wa magari hayo pamoja na kuzuia kwa muda wasindikizaji wa msiba kutoa maelezo zaidi.
“Jeshi la Polisi, kwa kushirikiana na viongozi wa serikali ya mtaa, waliingilia kati na kufanikisha kuwaokoa wasindikizaji wa msiba waliokuwa hatarini, huku hali ya usalama ikirejeshwa,” ilieleza taarifa ya polisi.