Wafugaji wilayani Simanjiro mkoani Manyara wameiomba serikali kuwasaidia namna ya kukabiliana na wimbi la wizi wa mifugo sambamba na tembo wanaofanya uharibifu kwenye maeneo ya malisho ya mifugo hiyo.
Kilio cha wananchi hao kimefikishwa kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Kamani ambaye licha ya kuiagiza Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro kushughulikia matatizo hayo pia amewataka wafugaji hao kuweka malengo ya muda mrefu ya kuwa na maeneo ya malisho kwa ajili ya mifugo yao ili kuondokana na adha ya kuyakosa nyakati za ukame.
“Sekta ya ufugaji ni miongoni mwa sekta muhimu kwa ustawi wa jamii na uchumi na hatuna sababu ya kutokuwa na uhakika wa malisho kipindi cha ukame hali inayotishia uhai na afya za mifugo yetu. Ni lazıma tuwe na malengo na mipango ya muda mrefu ya kuwa na malisho ya uhakika” amesema Naibu Waziri Ng’wasi Kamani.
Ameongeza kuwa ni wakati sasa wafugaji kufanya tathmini ya kuwa na maeneo yao na kujihakikishia uwepo wa malisho ya kutosha huku serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikiendelea kusambaza mbegu za malisho hayo kwa wafugaji.
Mwaka 2022 wilaya ya Simanjiro ilipoteza zaidi ya mifugo 62,500wakiwemo ng’ombe zaidi ya 35,000, kondoo zaidi ya 15,000, mbuzi zaidi ya 10,000 na punda zaidi ya 1,500 kutokana na ukosefu wa maji na malisho baada ya ukame kuvikumba baadhi ya vijiji vya wilaya hiyo iliyopo mkoa wa Manyara.
Imeandaliwa na @moseskwindi