OFISI ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) imewakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo kujadili na kutoa maoni kuhusu rasimu ya Mpango Mkakati wa Ofisi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2026/27 hadi 2030/31, kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi katika mamlaka za serikali za mitaa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho kilichofanyika leo Desemba 19, 2025 jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Profesa Tumaini Nagu, amesema kikao hicho ni sehemu ya mchakato mpana wa kuhakikisha Mpango Mkakati unaoandaliwa unazingatia uhalisia wa mahitaji ya jamii pamoja na mwelekeo wa kitaifa wa maendeleo.

Profesa Nagu amesema Serikali tayari imezindua Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inaendelea na maandalizi ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2026/27–2030/31) pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hivyo taasisi zote za umma, ikiwemo TAMISEMI, zinapaswa kuandaa mipango itakayochangia kikamilifu kufikia malengo hayo makubwa ya kitaifa.

Amefafanua kuwa kabla ya kuanza kuandaa Mpango Mkakati mpya, TAMISEMI ilifanya tathmini ya utekelezaji wa Mpango Mkakati unaomalizika muda wake mwezi Juni 2026, kwa kushirikisha Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na watendaji katika mamlaka za serikali za mitaa, vituo vya kutolea huduma za afya na shule.

“Kikao hiki ni mwendelezo wa vikao vingine vilivyotangulia, na lengo lake ni kupata maoni ya wadau kuhusu utekelezaji wa mpango unaomalizika pamoja na rasimu ya mpango unaoandaliwa, ili kubaini mafanikio, changamoto na maeneo yanayohitaji kuboreshwa,” amesema Profesa Nagu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *