Dar es Salaam. Wanamuziki wenye vipaji kila mara hutaka kuvitoa vipaji vyao hadharani ili visikike na ndivyo ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Muziki wa zamani ulikuwa mara nyingi ni wa vikundi si mtu mmoja mmoja kama ilivyo sasa. Na kulikuwa na vikundi vya muziki kila kona ya nchi, vikiporomosha muziki wenye mahadhi mbalimbali. 

Vingine vikielemea kwenye muziki wa magharibi vingine vikielemea Kongo na vingine vikibuni mitindo yao kutokana na muziki wa makabila yao. Katika  mchanganyiko huo na kukazaliwa vikundi vingi ambavyo vingine vilikuja kuwa maarufu sana. 

Vijana hasa waliokuwa sekondari walikuwa wanaanzisha vikundi vyao ambavyo vilikuwa vikipiga muziki wa kuelekea mapigo ya magharibi, wanamuziki waliweza kuiga na kupiga nyimbo za vikundi maarufu vya Ulaya na Marekani, kama vile Beatles, Temptations, The Famous Flames  na kadhalika.

Majina ya vikundi hivi nayo yalionesha kuwa yanaelemea muziki kutoka wapi. Tofauti na vikundi vya muziki vilivyokuwa vinapiga muziki kuelekea mapigo ya Kongo ambavyo majina yao yalikuwa na sifa ya kuwa Jazz Band au Orchestra kwa mfano, Western Jazz Band, Kilwa Jazz band, Orchestra Selesele, Orchestra Santa Fe. 

Vikundi vilivyokuwa vikipiga muziki uliokuwa ukiiga mapigo ya kimagharibi hata majina yao yalikuwa ya Kiingereza kwa mfano, The Sunburst, The Comets, Rifters, Jets, Sparks,  Revolutions na kadhalika. 

Zile bendi ambazo zilianza kwa mfumo wa kupiga muziki wa kimagharibi kisha zikahamia muziki wa rhumba majina yao yalibaki bila kujiita jazz band au orchestra  mfano Safari Trippers na Afro 70.

Kati ya bendi zilizokuwa na mfumo wa kuangalia magharibi kulikuweko na kundi lililoitwa The Rifters. Bendi hii lilianzishwa Dar es Salaam mwaka 1966 na Adam Kingui na mwenzie James Mwinga, vijana machachari wakati huo. 

Adam alidumu kwenye bendi mpaka pale ilipokuja kufutika. Bendi ilianza na wanamuziki wafuatao, Mlima akiwa kwenye gitaa la rhythm, Mudi kwenye gitaa la bezi, James Mwinga kwenye drums, baadaye Mohamed Mdoe akajiunga kama mpiga bezi lakini baadaye akahamia kupiga drums. 

Raphael Sabuni akiwa anapiga gitaa la solo na gitaa la  rhythm. Kadri muda ulivyoenda kukawa na mabadiliko na Kingui aliwaingiza katika kundi lake wanamuziki wengine vijana kama akina Ebby Sykes, Nasoro “Mick Jagger” Fadhili kwenye gitaa la bezi, Khalid Mosty kwenye drums na mwanamuziki toka Afrika ya Kusini Vuli Yeni, akiwa mwimbaji, huyu Vuli hatimaye akaja kujiunga na kundi la Lucky Dube. 

Kingui pia akamkaribisha mpiga gitaa la rythm Belino. Kundi la Rifters lilikuwa likiandaa maonesho yaliyoitwa Tammi Shows katika ukumbi wa Splendid Hotel, ambapo pamoja na muziki kulikuwa na wacheza show, jambo ambalo linapinga nadharia ya muda mrefu kuwa stage show zilianza baada ya safari ya Franco Tanzania mwaka 1973 Mwaka 1975 Adam Kingui na Nasoro Fadhili waliondoka nchini na kuelekea Mombasa ambako waliendelea na shughuli za muziki. 

Kwa bahati mbaya bendi hizi ambazo zilikuwa zikipiga muziki wenye mlengo wa magharibi hazikuwa maarufu kwa kurekodi nyimbo zao, hivyo picha na hadithi zao tu ndio zimebaki, lakini zile ambazo zilirekodi zimeacha alama kubwa ya kudumu ambayo bado inaheshimika. 

Kati ya bendi zilizorekodi ilikuwa bendi ya Sunburst ambayo ilikuwa na mchanganyiko wa wanamuziki kutoka Tanzania, Nigeria na Kongo, bendi hii ilirekodi nyimbo zao Tanzania na Zambia na kampuni ya Strut Records imeanza kuzisambaza upya kazi hizi ambazo wanamuziki wake wengi hawapo tena duniani. 

Kundi la Sunburst lilianzishwa mwaka 1970 na mwanamuziki mwenye asili ya Kongo aliyeitwa Hembi Flory, yeye akawakusanya wanamuziki wenzie kama mpiga drum Johnny ‘Rocks’ Fernandes huyu ana asili ya Kigoa, mpiga bass Bashir Idd Farhani, na mpiga kinanda Kassim Magati, mwimbaji James Mpungo kijana kutoka Mbeya ambaye baadaye alikuja kujiunga na Les Mangelepa nae akajiunga na Sunburst pia.

Kundi hili lilikuwa likipiga mtindo wa Afro Rock na mwaka 1973 kundi hili lilishinda mashindano ya Bendi Bora yaliyofanyika Dar es Salaam, katika mashindano hayo bendi ya Tonics ilikuwa ya pili na Safari Trippers ikawa ya tatu. 

Wanamuziki wengine waliokuwa katika kundi hili ni Toby John Ejuama mpiga saksafon aliyekuwa Mnaijeria kutoka jimbo la Biafra. Katika maelezo haya ya vikundi viwili tu, nimeweza kutaja majina ya wanamuziki wawili ambao walikuja kujiunga kwenye makundi ya muziki ambayo yaliweza kuja sifika katika ulimwengu wa muziki.  

James Mpungo aliyekuja kujiunga na Les Mangelepa na Vuli Yeni aliyejiunga na kundi la Lucky Dube. Kuna wanamuziki wengine kadhaa walikuja kuonyesha umahiri wao nje ya mipaka ya nchi yetu kuonyesha kuwa kiwango walichokuwa wanafikia kilikuwa kinakubalika hata nje ya nchi yetu. 

Historia ya wanamuziki wa Tanzania ina mengi ya kujivunia kama Taifa lakini bado yamejificha

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *