Dar es Salaam. Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Abdalla Hamid amesema CCM kitayafikia makundi yote ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili kuwapa misaada ya kujikimu kimaisha.
Rabia ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Desemba 20,2025 wakati akitoa misaada mbalimbali ikiwemo vyakula na vifaa vya shule kwa watoto wanaoshi mazingira magumu katika kituo cha Malaika Kids, Kinondoni Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Rabia, kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka CCM kimeamua kuwapata tabasamu watoto wa Tanzania, wakianzia katika kituo cha Malaika Kids.
“Nimetumwa na chama changu kuleta tabasamu katika kituo hiki cha cha Malaika Kids, nikiwa kama mkuu wa idara wa mambo ya siasa na uhusiano wa kimataifa, ninajukumu pia la kufuatilia maendeleo ya jamii.
“Nimeelekezwa kukabidhi zawadi kwa watoto wetu hasa wanaoshi katika mazingira magumu.Niwahakikishie CCM itaendelea kuyafikia makundi yote katika jamii ya Watanzania,” amesema Rabia.
Rabia amesema Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi tabasamu, hivyo wasaidizi wake wameanza kulitekeleza kwa kuanzia kwa watoto wa kituo hicho.
Mwanzilishi Mwenza Malaika Kids, Charles Nyimbo ameishukuru CCM kwa kuwakumbuka watoto wanaoishi kituoni hapo.
“Tunakishukuru Chama Cha Mapinduzi CCM kwa msaada huu, pia tunatambua upendo alionao Rais Samia kwa watoto wa Taifa hili,” amesema Nyimbo.