
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imelaani shamulizi la kikatili la Israel dhidi ya shule moja katika mji wa Gaza lililouwa Wapalestina kadhaa. Hamas imeitaja hujuma hiyo kuwa jinai ya kivita ya makusudi na ukiukaji wa wazi wa mapatano ya kusitisha mapigano.
Taarifa ya Hamas iliyotolewa leo Jumamosi imekosoa kimya cha jamii ya kimataifa kuhusu uhalifu huo wa Israel na kushindwa kuzuia jinai zinazofanywa na utawala huo dhidi ya watu wa Gaza.
Taarifa ya Hamas imeeleza kuwa: “Mashambulizi ya mizinga yaliyofanywa na jeshi la utawala ghasibu wa Israel katika shule inayohifadhi raia wa Paletsina waliokimbia makazi yao katika kitongoji cha Al-Tuffah, mashariki mwa mji wa Gaza na kuuwa shahidi raia kadhaa, wengi wao wakiwa ni watoto, ni jinai ya kikatili dhidi ya raia wasio na hatia na ukiukaji wa mara kwa mara wa makubaliano ya kusitisha mapigano.”
Taarifa ya Hamas imeongeza kuwa: Utawala gaidi wa Israel unaendelea kukiuka kwa makusudi mapatano ya kusitisha mapigano huku ukiwalenga raia katika Ukanda wa Gaza.
Wapalestina zaidi ya 400 wameuliwa shahidi katika mashambulizi ya Israel tangu kutangazwa mapatano ya kusitisha mapigano zaidi ya miezi miwili iliyopita huku kukiwa na ukimya wa kimataifa na kushindwa kuchukua hatua dhidi ya uhalifu huo.
Hamas pia imesistiza kuwa utawala ghasibu wa Israel hauishii katika kuwashambulia raia, bali unazidisha janga la binadamu kwa kuzuia magari ya ambulensi na timu za wataalamu wa afya kufika katika maeneo ya mashambulizi ili kuokoa na kutibu majeruhi.