
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeilaani vikali Marekani kwa kuviwekea vikwazo majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ikisema Washington inalinda waliotenda makosa makubwa ya jinai.
Katika chapisho kwenye mtandao wa X, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amesema hatua hiyo imefichua udhaifu wa kina wa maadili katika sera za Marekani.
Ameongeza kuwa: “Wakati wahalifu wa vita vya mauaji ya kimbari wakiendelea kutembea huru na kuendeleza ukatili wa kutisha dhidi ya ubinadamu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inaongeza shinikizo na kuwawekea vikwazo wale wanaojitahidi kuwawajibisha wahalifu hawa.” Aidha amesema: “Hii ni sura ya wazi na ya kikatili ya ukwepaji adhabu—upotovu mkubwa wa maadili.”
Kauli hiyo imekuja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, kutangaza Alhamisi vikwazo dhidi ya majaji wawili wa ICC: Gocha Lordkipanidze kutoka Georgia na Erdenebalsuren Damdin kutoka Mongolia.
Mahakama ya ICC, yenye nchi wanachama 125, imekuwa ikikabiliwa na shinikizo linaloongezeka kutoka Washington. Mnamo Februari, Ikulu ya White House iliweka vizuizi dhidi ya mahakama hiyo, ikidai kuwa ilikuwa ikijibu kile ilichokiita “hatua zisizo halali” zinazolenga Marekani na Israel.
Vikwazo hivyo, vilivyowekwa kupitia amri ya kiutendaji ya Rais wa Marekani Donald Trump, vinazuia upatikanaji wa huduma muhimu na kuzuia kuingia Marekani. Hatua hizo zilichochewa na uamuzi wa ICC kutoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wake wa zamani wa masuala ya vita Yoav Gallant, kwa “makosa dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita” katika vita vya mauaji ya kimbari Gaza.
Tangu Oktoba 2023, jeshi la Israel limewaua zaidi ya Wapalestina 70,660—wengi wao wakiwa wanawake na watoto—na kuwajeruhi wengine 171,000 katika vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelea Gaza. Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameelezea vita hivyo, vinavyowezeshwa kwa kiasi kikubwa na msaada wa kijeshi na kisiasa wa Marekani, kuwa ni mauaji ya kimbari.