
-
- Author, Anthony Zurcher
- Nafasi, BBC
-
Muda wa kusoma: Dakika 7
Katika mkutano wa baraza lake la mawaziri katika Ikulu ya White House wiki mbili zilizopita, Rais wa Marekani Donald Trump katika chumba kilichojaa washauri wake wakuu, maafisa wa utawala na wasaidizi, na akatoa utabiri, mgombea urais wa chama cha Republican anayefuata, “labda ameketi hapa.”
Licha ya marekebisho ya katiba yanayomwekea kikomo cha mihula miwili ya miaka minne, wafuasi wake waliimbia “miaka minne tena” katika mkutano wa hadhara Jumanne iliyopita huko Pennsylvania.
Katika chumba cha baraza la mawaziri wiki iliyopita, alipokuwa akizungumzia juu ya uteuzi wa rais wa Republican 2028, aliweka wazi: “Sitakuwa mimi.”
Katika uchaguzi wa mitaa wa mwezi uliopita, Chama cha Republican kilipoteza uungwaji mkono miongoni mwa wapiga kura wachache na wafanyakazi waliomsaidia Trump kushinda kurudi tena Ikulu ya White House 2024.
Wajumbe wa timu yake wametofautiana kuhusu sera. Na baadhi, hasa Mbunge Marjorie Taylor Greene, wamejiondoa kwenye kundi la Trump, wakimtuhumu rais kwa kupoteza mawasiliano na Wamarekani waliompa madaraka.
Kumekuwa na uvumi kuhusu mpasuko wa Maga (Make America Great Again) katika baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa, na pia nyumbani.
Siku ya Jumatatu, kichwa cha habari katika gazeti la The Washington Post kiliuliza: “Viongozi wa Maga wanamwonya Trump kwamba wafuasi wanaondoka. Je, atasikiliza?”
Nani Mrithi wa Trump?
Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
Makamu wa Rais JD Vance aliketi karibu na rais. Anachukuliwa kama mrithi anayetarajiwa zaidi wa Trump.
Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio alikuwa upande wa kulia wa rais. Ni Seneta huyo wa zamani wa Florida, ambaye alishindana na Trump katika uteuzi wa chama cha Republican mwaka 2016.
Ameacha kuunga mkono sera ya uhamiaji huria na msimamo wake mkali dhidi ya Urusi na kuunga mkono sera ya Trump ya America First. Lakini ikiwa kuna mtu yeyote wa Republican mwenye ushawishi katika chama cha Trump, Rubio anaongoza orodha.
Kisha kuna Waziri Robert F Kennedy Jr, ambaye ana shaka kuhusu chanjo na ajenda yake ni “Make America Healthy Again,” aliketi karibu na Rubio. Yeye ni kutoka chama cha Democratic lakini aliyegeuka kuwa mwanasiasa huru na kisha kuwa Republican.
Na hatimaye, Kristi Noem, waziri wa usalama wa ndani. Ingawa gavana huyo wa zamani wa South Dakota hachukuliwi kama mgombea wa urais ajaye, lakini utetezi wake wa utekelezwaji wa sera kali za uhamiaji – ikiwa ni pamoja na wito wake wa hivi karibuni wa marufuku ya usafiri kwa “kila nchi ambayo imekuwa ikilijaza taifa letu wauaji na wanyonyaji” – kumemfanya kuwa sura maarufu juu ya sera za utawala huo.
Republican iliyobadilishwa
Chanzo cha picha, Getty Images
Bila shaka hakuna hata moja kati ya hayo lenye uhakika – wala hakuna uhakika kwamba kizazi kijacho cha viongozi wa Maga kitatokana na mtu kutoka karibu na rais. Trump alivamia Ikulu ya White House kama mgeni wa kisiasa. Kiongozi anayefuata wa Republican anaweza kuwa mvamizi kama Trump.
“Itakuwa juu ya rais ajaye wa Republican kufuata nyayo za Trump au kujitenga naye,” anasema Mbunge wa zamani wa Republican Rodney Davis wa Illinois, ambaye sasa anafanya kazi katika Chama cha Biashara cha Marekani.
Uchaguzi wa urais wa Novemba 2028 utakapo aanza, wapiga kura wa Marekani huenda hata wasimtake mtu kama Trump. Baadhi ya kura za maoni ya umma zinaonyesha rais huenda asiwe maarufu kama alivyokuwa hapo awali.
Utafiti uliofanywa na YouGov mapema mwezi huu ulionyesha rais ana kiwango cha kukubalika cha -14, ikilinganishwa na +6 alipochukua madaraka Januari. Kisha kuna wasiwasi kuhusu uchumi na juhudi zake zisizokoma za kwenda nje ya mipaka ya madaraka ya rais.
Uongozi wa Trump bado unawakilisha funguo za himaya ya Republican, hata kama himaya hiyo imebadilika sana katika miaka ya hivi karibuni.
“Nadhani Republican imekuwa tofauti kimsingi katika miongo michache iliyopita,” anasema Davis, ambaye alihudumu katika Bunge kuanzia 2013 hadi 2023. “Republican ya wakati wa Ronald Reagan alipochaguliwa si Republican ya leo.”
Huko nyuma katika miaka ya 1980, sera za Reagan zilikuwa ni mchanganyiko wa uchumi wa soko huria, uhafidhina wa kitamaduni, kupinga ukomunisti na masuala ya kigeni, anasema Laura K Field, mwandishi wa Furious Minds: The Making of the Maga New Right.
Tofauti na enzi ya Reagan, kanuni kuu za Trump ni pamoja na “kulinda mipaka, utaifa wa kiuchumi na sera ya kigeni ya Marekani kwanza.”
‘Warepublican wa aina mbili’
Chanzo cha picha, Getty Images
Mapema mwezi huu, Taasisi ya mrengo wa kihafidhina ya Manhattan ilitoa utafiti juu ya wapiga kura wa Republican, na kutoa mwanga zaidi kuhusu Trump.
Ilieleza kwamba 65% ya wafusi wa Chama cha Republican kwa sasa ni wale “Warepublican kindakindaki” – ambao wamemuunga mkono rais tangu 2016. (Kama wangekuwa hai katika miaka ya 1980, huenda wangempigia kura Reagan.)
Kwa upande mwingine, 29% ni kile ambacho Taasisi hiyo inasema ni “Warepublican wapya wanaoingia.” Ndio Warepublican wapya ambao wanaleta changamoto.
Ni zaidi ya nusu tu ya hao ndio walisema wataiunga mkono Republican katika uchaguzi wa katikati ya muhula wa bunge mwaka ujao.
Kulingana na utafiti huo, hao wapya ni vijana, wako tofauti na wana uwezekano mkubwa wa kuwa na maoni yanayokinzana na imani za kihafidhina.
Wana maoni yanayoegemea mrengo wa kushoto kuhusu sera za kiuchumi, huwa na mwelekeo wa kutaka kuwepo uhuru zaidi kuhusu masuala ya uhamiaji na kijamii, na pia huwa na msimamo mkali dhidi ya China au kuikosoa Israeli.
Jesse Arm, makamu wa rais katika Taasisi ya Manhattan, ameimbia BBC katika barua pepe: “Mazungumzo mengi kuhusu mustakabali wa chama hicho yanaendeshwa zaidi mtandaoni, badala ya wapiga kura ambao kwa kweli wanaunda sehemu kubwa ya muungano wa Republican.”
Labda haishangazi, wapiga kura wapya wa Republican wanaojiita wapiga kura wapya hawawaungi mkono sana baadhi ya warithi watarajiwa wa Trump. Ingawa 70% ya Warepublican kindakindaki wana maoni chanya kuhusu Rubio na 80% kwa Vance, ni nusu tu ya wapiga kura wapya wana maoni chanya kuhusu watu hao.
Mambo mengine ni kwamba: Zaidi ya nusu ya wapiga kura wapya wanaamini matumizi ya vurugu za kisiasa katika siasa za Marekani “wakati mwingine yanafaa” – ikilinganishwa na 20% tu miongoni mwa Warepublican kindakindaki.
Hili kundi jipya pia inaonyesha kuwa wana uwezekano mkubwa wa kuvumilia kauli za kibaguzi au chuki dhidi ya Wayahudi na wana mwelekeo zaidi wa kuwa na mawazo ya njama – kuhusu mada kama vile kutua mwezini, 9/11 na chanjo.
Trump aliweza kuwavutia wapiga kura hawa. Swali ni kama yeye na warithi wake wa kisiasa wanaweza kuwabakisha.
“Mwisho wa siku, moyo wa chama unabaki kwa wa-Republican kindakindaki, sio wale wa pembeni wanaosikika kupitia vyombo vya habari.”
Mivutano ya wahafidhina
Chanzo cha picha, Reuters
Ugomvi kati ya Trump na Greene uliosababisha kujiuzulu kwa Greene kutoka Bunge ulianza kwa kuunga mkono kutolewa kwa faili zinazohusiana na kesi ya biashara haramu ya ngono na watoto ya Jeffrey Epstein.
Hata hivyo, ulipanuka kutokana na ukosoaji wa sera ya Trump juu ya Mashariki ya Kati na shutuma za kushindwa kwake kushughulikia masuala ya gharama za maisha na huduma za afya kwa wapiga kura wa Marekani wenye kipato cha chini.
Mgawanyiko wa awali wa Maga ulizuka kuhusu sera ya kiuchumi ya Trump, huku bilionea Elon Musk, mfuasi mkubwa na mwanachama wa karibu wa Trump, akilaani baadhi ya ushuru na sera na matumizi ya serikali.
Kwa sasa, rais amejaribu kwa kiasi kikubwa kujiepusha na mzozo mwingine mkali ndani ya safu za wahafidhina kuhusu kama Nick Fuentes, mchambuzi wa siasa kali za mrengo wa kulia, anakaribishwa katika harakati za wahafidhina.
Katika ukumbi wa Bunge linalodhibitiwa na Republican, dalili za msuguano zinaonekana. Licha ya ushawishi wa Ikulu, haikuweza kuzuia Baraza hilo kutopitisha muswada wa kutolewa kwa faili za Epstein.
Wakati huo huo, chama cha Trump kimekuwa kikishindwa katika uchaguzi, huku chama cha Democrats kikishinda ugavana huko Virginia na New Jersey mwezi uliopita kwa kura nyingi.
Katika chaguzi kadhaa maalum zilizopingwa kwa viti vya majimbo na vya mitaa katika mwaka uliopita, Democratics kwa wastani wameboresha kiwango chao cha ushindi kwa karibu 13% ikilinganishwa na chaguzi kama hizo zilizofanyika katika uchaguzi wa kitaifa wa Novemba mwaka jana.
Mustakabali wa Utawala wa Trump
Chanzo cha picha, Getty Images
Haya yote yatakuwa mawazoni mwa Warepublican kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa bunge wa 2026 – na hayatasaidia sana kupunguza wasiwasi unaowakabili baadhi ya watu.
Hata hivyo, hata ikiwa watashindwa mwaka ujao – au mwaka 2028 – hakuna uwezekano wa kuashiria mwisho wa Utawala wa Trump.
Lakini mabadiliko ambayo Trump ameyafanya ndani ya Chama cha Republican chenyewe yanaonekana kuwa ya msingi, kulingana na Bi Field.
Muungano wake wa Maga unajengwa juu ya aina ya harakati za watu wengi nchini Marekani ambazo zilianza miongo kadhaa au zaidi – kuanzia kampeni ya urais ya Barry Goldwater mwaka wa 1964 hadi maandamano ya Chama cha Tea wakati wa urais wa Barack Obama.
“Harakati za Trump ziko hapa kwa muda mrefu na hakuna uwezekano wowote wa Republican ya zamani kurudi na aina yoyote ya ushawishi – hilo liko wazi.”