
Dar es Salaam. Waandishi wa habari waliopo katika Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) wametakiwa kuwa wazalendo na nchi yao kabla ya kuandika au katangaza habari yoyote.
Sambamba na hilo pia wametakiwa kujenga uaminifu mbele ya umma, ili kuweza kuaminiwa na kujitofautisha na watu wengine.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Tumaini Media, January Nchimbi katika ufunguzi wa mafunzo ya siku kumi kwa waandishi wa taasisi hiyo, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam ambapo alikuwa mgeni rasmi.
“Tukumbuke tunapoandika habari kuwa wazalendo wa nchi yetu, hata nchi nyingine ndivyo zinavyofanya, mchuje kitu gani cha kuandika na ambacho sio cha kuandika ili kuiacha nchi salama.
“Lakini pia katika uaminifu, mkumbuke JMAT ni taasisi ya usuluhishi kwa jamii, hivyo waandishi wake pia lazima waaminiwe ili inapotokea mgogoro wowote muaminiwe kuwa mnaweza kuusuluhisha bila kuegemea upande wowote,” amesema Nchimbi.
Akizungumzia mafunzo hayo, aliwataka wanahabari hao kuwa makini katika kusikiliza kwa kuwa tayari tasnia ya habari imeundiwa sheria nyingi, ambazo wanapaswa kuzielewa vizuri ili kuepuka kuingia katika matatizo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
“Kuna sheria imetungwa kwa ajili ya waandishi, hivyo katika mafunzo haya msikilize kwa makini nini kinachotakiwa katika uandishi na kuuliza maswali kadri muwezavyo, ili kupata uwelewa mpana katika tasnia hiyo,” amesema Nchimbi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa JMAT, Ayoub Sanga amesema wametoa mafunzo hayo ambayo yameratibiwa na kamati ya habari, mahusiano na uenezi ya Jumuiya hiyo, wakiamini taasisi hiyo itafika mbali kama itazidi kuikumbatia elimu.
“Pamoja na mambo mengine, tunaamini kuwa na sisi tunahitaji elimu ya masuala ya habari licha ya kuwa tuna zaidi ya idara 17, ikiwemo ile ya mazingira, ustawi wa jamii, fedha, uwekezaji, afya na tiba, wazee, usimamizi na uwajibikaji na ulinzi, usalama na itifaki.
“Mambo yote haya ili kuyafanyia kazi ni wazi kuwa yanahitaji maarifa na taaluma, hivyo hatujafanya kosa kuwakutanisha leo watu wetu hapa,” amesema Sanga.
Awali, Katibu wa JMAT Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Yassin Masenga, akimwakilisha Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Sheikh Alhad Mussa amesema wanahabari 150 watapata mafunzo hayo yanayotolewa kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Uandishi wa Habari (IJMC).
Amesema mpango huo unao lenga kuimarisha uandishi wenye maadili huku kaulimbiu ikiwa ni ‘uandishi kwa maadili, maridhiano na amani’.
Kaulimbiu hiyo, amesema inamaanisha kuwa kalamu na mawasiliano ina nguvu kubwa katika kujenga au kubomoa jamii.
“Hivyo kupitia mafunzo haya tunalenga kuwakumbusha na kuwawezesha waandishi na watumiaji wa mawasiliano kuandika kwa ukweli, uwajibikaji na uzalendo, wakizingatia masilahi mapana ya jamii na Taifa.
Kwa upande wao wanahabari, Sylivia Chilolo amesema anajisikia faraja kuwa miongoni mwa wanaopata mafunzo hayo, kwa kuwa anaamini mwanahabari bado anahitajika kujua vitu vingi katika tasnia hiyo ikizingatia dunia kila leo inakuja na mambo mapya.
Naye mwanahabari Baraka Kasima amesema kupata elimu siku hizi ni gharama, lakini wanashukuru JMAT kuwagharamia kuipata na kuahidi watakapomaliza watayafanyia kazi yale watakayokuwa wamefundishwa kwa faida ya wananchi na tasnia kwa ujumla.