
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe, amethibitisha kwamba Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) kuanzia mwaka 2028 na kuendelea zitakuwa zikichezwa kila baada ya miaka minne.
Hatua hii inaashiria mabadiliko makubwa katika soka la Afrika, ikilenga kupunguza migongano ya muda na kalenda ya kimataifa ambayo imekuwa sugu kwa miaka mingi.
Akizungumza Rabat leo, Motsepe amesema kuwa uamuzi huo wa Kamati ya Utendaji ya CAF unalenga kuyapa thamani mashindano hayo.
“Kwa taarifa tu, mwaka 2027 tutaenda Tanzania, Kenya na Uganda. AFCON itakayofuata, kama sehemu ya mabadiliko haya ya kimataifa, wachezaji bora wa Kiafrika… watashiriki na tutaamua mahali fainali itakapofanyika Afrika Kaskazini.
“tutakuwa na mashindano yanayofanana na AFCON kila mwaka, yakihusisha wachezaji nyota wanaocheza soka la Afrika katika kiwango cha juu kabisa cha bara kila mwaka,” amesema Motsepe.
Ili kudumisha mwendelezo wa mashindano katika kipindi hiki cha miaka minne, CAF itazindua Ligi ya Mataifa ya Afrika (African Nations League) kila mwaka kuanzia 2029.
Marekebisho haya yanakuja baada ya miaka ya mvutano mkali kati ya CAF, Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) na klabu za Ulaya.
Mashindano ya mwaka 2025 yalisogezwa hadi Desemba ili kuepuka kugongana na Kombe la Dunia la Klabu la FIFA katika majira ya kiangazi.
Klabu za Ulaya, ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikisita kuwaachia wachezaji wao muhimu katikati ya msimu, ziliishinikiza FIFA kuchelewesha tarehe ya lazima ya kuwaachia wachezaji hadi Desemba 15, siku sita tu kabla ya mashindano kuanza.
Uamuzi huu ulizua ukosoaji mkali kutoka kwa makocha wa Afrika, waliotahadharisha kuwa muda mfupi wa maandalizi unaharibu mipango ya mazoezi ya timu za taifa.
Mabadiliko haya yanaongeza mtikisiko wa zaidi ya muongo mmoja kwa mashindano haya, ambayo yameongezeka hadi timu 24 na wakati wake kubadilishwa kati ya Januari na Juni ili kudhibiti changamoto za hali ya hewa na shinikizo kutoka kwa klabu.
Katika hatua nyingine, CAF imetangaza ongezeko la zawadi kwa bingwa wa mashindano hayo.
Baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya CAF kilichofanyika mapema leo, shirikisho hilo limethibitisha ongezeko lingine la juu katika muundo wa zawadi ambapo bingwa kuanzia sasa atapata Dola 10 milioni (Sh25 bilioni).
Hatua hii inaonyesha mkakati wa muda mrefu wa CAF wa kulifanya soka la Afrika kuwa endelevu na lenye ushindani wa kibiashara katika kiwango cha kimataifa.
Kabla ya hapo, bingwa alikuwa anapata Dola 7 milioni (Sh17.5 bilioni) na mshindi wa pili Dola 4 milioni.