Dar es Salaam. Tanzania inaendelea kurekodi ongezeko la mauzo ya bidhaa zake katika masoko ya nje mwaka hadi mwaka, hali inayoakisi kuimarika kwa uchumi  na mchango wa sekta mbalimbali katika upatikanaji wa fedha za kigeni.

Kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kuna maeneo matano makuu yanayoingiza mapato makubwa zaidi ya fedha za kigeni nchini.

Maeneo hayo ni dhahabu, utalii, usafirishaji, bidhaa za viwandani na tumbaku.

Kwa pamoja, sekta hizi zimeliingizia Taifa jumla ya Sh33.485 trilioni katika mwaka wa fedha ulioishia Oktoba mwaka huu, ikiwa ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na Sh27.828 trilioni zilizopatikana katika kipindi kama hicho mwaka uliotangulia.

Dhahabu imeendelea kuongoza kwa kuingiza mapato makubwa zaidi, ikichangia Sh11.469 trilioni, ikifuatiwa na sekta ya utalii iliyochangia Sh10.724 trilioni.

Sekta ya usafirishaji iliingiza Sh6.164 trilioni, bidhaa za viwandani Sh3.885 trilioni, huku tumbaku ikichangia Sh1.241 trilioni.

Akizungumzia mwelekeo huo, mtaalamu wa uchumi Profesa Aurelia Kamuzora amesema kuwa kilimo ni miongoni mwa sekta zinazofanya vizuri katika kuingiza fedha za kigeni, licha ya mchango wake kutojitokeza wazi katika takwimu rasmi.

Amesema hali hiyo inatokana na changamoto za mnyororo wa thamani kutobainishwa ipasavyo, kwani mara nyingi bidhaa za kilimo zinapoongezewa thamani, mchango wa sekta hiyo hauonekani moja kwa moja, huku sehemu inayozalisha bidhaa ya mwisho ndiyo hutambulika kama chanzo kikuu cha mapato.

“Ninaamini mchango wa sekta ya kilimo ni mkubwa sana, lakini changamoto iliyopo ni kwamba hesabu zake hazijapigwa kwa usahihi.

“Ili kubaini ukweli wa jambo hili, angalia kinachotokea pale kilimo kinapoondolewa; itakuwa vigumu kuona utendaji wa viwanda mbalimbali, ikiwemo vya tumbaku na sukari,’’ amesema.

Ameongeza: “Unaposema mchango wa viwanda vya sukari ni mkubwa, ondoa kwanza miwa uone kama mchango huo bado utaonekana.

“Hali hii inaonesha wazi kuwa kilimo, ambacho mara nyingi huhesabiwa mwisho katika mnyororo wa thamani, kimekuwa kikitoa mchango mkubwa lakini usiotambulika ipasavyo, jambo linalosababisha mchango wake kutoonekana bayana.’’

Amesema jambo hilo likibadilishwa linaweza kusaidia kuongeza hamasa ya watu wanaotaka kuingia katika kilimo tofauti na sasa.

“Ukikata kilimo Tanzania haipo, kutoongeza thamani katika madini ndiyo inafanya mchango wake kuonekana ni mkubwa lakini ni hasara. Nadhani zingekuja takwimu kuonyesha mchango wa kilimo katika mnyororo wa thamani wa kilimo tutaona thamani yake,” amesema.

Amesema ili kujua mchango wa sekta nyingine ni vyema kuangalia mnyororo mzima wa thamani na namna zinavyochangia katika kuwezesha sekta nyingine.

“Madini yanaonekana kufanya vizuri kwa sababu yanauzwa kama malighafi hayaongezewi thamani ingekuwa kuna kiwanda cha kuongeza thamani ingekuwa inahesabiwa bidhaa ya mwisho na viwanda ndiyo vingeonekana kufanya vizuri,” amesema.

Akielezea kwa nini maeneo hayo matano ndiyo yamekuwa yakijirudia kila wakati kwa kuleta fedha nyingi, mtaalamu wa uchumi Dk Goodhope Mkaro amesema hiyo inatokana na wingi wa bidhaa na upatikanaji.

Ametolea mfano wa dhahabu kufanya vizuri wakati wote akisema ni kwa sababu inapatikana kwa wingi na inahitajika sokoni huku utalii nao  rasilimali zake zikiwepo.

“Lakini kwa upande mwingine, hatuna bidhaa nyingi zinazohitajika kwa kiwango kikubwa na masoko ya nje.

“Badala yake, tunaendelea kuagiza bidhaa nyingi zaidi kuliko tunavyouza nje, hali inayosababisha ongezeko kubwa la mapato kuonekana zaidi katika sekta za huduma kama utalii, ambako idadi ya wageni wanaoingia nchini inaendelea kuongezeka,” amesema.

Kuhusu huduma kufanya vizuri, takwimu zinaonyesha kuwa ukuaji wa mapato utalii kulitokana na ukuaji thabiti wa sekta hiii, huku idadi ya watalii ikiongezeka kwa asilimia 11.4 hadi kufikia watalii 2,324,387.

Mmoja wa watembeza watalii alipozungumza na Mwananchi, Benard Lukonja amesema sekta hiyo ipo katika nafasi ya kufanya vuziri zaidi kuliko dhahabu ikiwa nguvu ya utangazaji katika masoko yenye watu wengi zaidi ikaongezeka.

“Kuna nchi ambazo bado hatujazifikia vizuri, nchi kama India tukitangaza vizuri kulingana na idadi yao ya watu tunaweza kupata wageni wengi kutoka huko na hili lifanyike wakati ambao nchi inaweka utaratibu wa kuondoa viza kwa wageni ambao wanataka kuingia huku,”

“Bila kufanya hivi itakuwa ni ndoto au kama viza watalipia basi iwe rahisi kupatikana hata mtandaoni ndani ya saa 24 siyo mtu asubiri kwa miezi mingi inakatisha tamaa kwa kweli,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *