Chanzo cha picha, Getty Images
Marekani imesema jeshi lake limeanzisha “shambulio kubwa” dhidi ya kundi la Islamic State (ISIS) nchini Syria, kufuatia shambulio la hivi karibuni lililowaua wanajeshi kadhaa wa Marekani.
Kamandi ya kijeshi ya Marekani ya Centcom imesema ndege za kivita, helikopta za kushambulia na mizinga zilishambulia zaidi ya maeneo 70 ya katikati mwa Syria.
Ndege za kijeshi za Jordan pia zilishiriki katika operesheni hiyo. Centcom ilisema operesheni hiyo ilitumia zaidi ya silaha 100 za viwango vya juu, zikilenga miundombinu ya kifedha ya ISIS na maeneo ya silaha.
Rais Donald Trump alisema alikuwa “anashambulia kwa nguvu kubwa” maeneo muhimu ya ISIS, kufuatia shambulio la kundi hilo la tarehe 13 Desemba katika mji wa Palmyra, lililoua wanajeshi wawili wa Marekani na mkalimani mmoja raia wa Marekani.
Katika taarifa iliyowekwa kwenye X.com, Centcom inayosimamia operesheni za kijeshi za Marekani barani Ulaya, Afrika na eneo la Indo-Pasifiki ilisema operesheni iliyopewa jina la “Hawkeye Strike” ilianza jana Ijumaa.
Kamanda wa Centcom, Admiral Brad Cooper, alisema Marekani “itaendelea kuwafuatilia bila kuchoka magaidi wanaolenga kuwadhuru Wamarekani na washirika wetu katika eneo hili.”
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, alisema operesheni hiyo “si mwanzo wa vita bali ni tamko la kulipiza kisasi.” Aliongeza: “Iwapo mtawashambulia Wamarekani popote duniani mtatumia maisha yenu mafupi na yenye hofu mkijua kwamba Marekani itawawinda, itawapata, na itawaua bila huruma.”
“Leo, tumewawinda na kuwaua maadui wetu. Wengi wao. Na tutaendelea kufanya hivyo,” aliongeza waziri huyo wa ulinzi. Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa Truth, Rais Trump alisema Marekani “italipiza kisasi kikali sana, kama nilivyoahidi, dhidi ya magaidi wauaji waliokuwa nyuma ya shambulio la Palmyra.”
Alisema pia kuwa serikali ya Syria “inaunga mkono kikamilifu” operesheni hiyo.
Soma zaidi: