Dar/Mikoani. Sikukuu za mwishoni na mwanzoni mwa mwaka ni fursa kwa wana jamii kukusanyika, kukumbuka walikotoka na kujiuliza wanakoelekea.

Wapo wanaosafiri kurudi nyumbani, na wengine huongeza mawasiliano ya salamu baina yao na hata milango ya nyumba iliyofungwa kwa miezi kadhaa, hufunguliwa kwa ajili ya wageni.

Katika mikusanyiko hii, zipo simulizi za mafanikio, kila mmoja na hadithi yake. Aliyeajiriwa husimulia alivyopanda cheo, mfanyabiashara hueleza faida na hasara za mwaka na kijana anayejitafuta hutaja ndoto anazozifukuzia.

Hata hivyo, katikati ya vicheko na pongezi, kuna maswali yasiyokwepeka ambayo wakati mwingine huulizwa kwa njia ya utani, lakini yakibeba uzito wa matarajio ya kijamii.

“Bado hujaoa? Au harusi lini?” ni miongoni mwa maswali yanayoulizwa kwa mzaha, lakini masikioni mwa mhusika ni kama vile anahukumiwa.

Kwa wengine maswali haya ni kichocheo cha tafakuri, huku kwa baadhi ni chanzo cha msongo wa mawazo.

Penye wengi pana mengi, wapo wanaorudi nyumbani lakini hawakai, wao kutwa ni kiguu na njia. Hutumia mapumziko ya sikukuu kushinda baa, wakikumbatia vinywaji na marafiki, wakiwemo waliotoka nao mijini.

Kwao, kelele za muziki na vicheko vya mezani ni mbadala wa ukimya nyumbani unaoambatana na maswali wasiyokuwa tayari kuyajibu.

Teknolojia nayo imezua jambo katika mikusanyiko hii. Ndani ya sebule iliyojaa watu, kila mmoja anaweza kuwa peke yake. Simu mkononi, macho kwenye skrini, mazungumzo yakikatizwa mara kwa mara.

Kwa wazee huachwa na bumbuazi wakijiuliza: “Ni kwa nini vijana wako pamoja kimwili lakini hawapo kiakili.”

Kwa vijana, ulimwengu wa mtandaoni ni sehemu ya maisha yao, mahali pa kujenga mahusiano, kujifunza na hata kukimbia hisia zisizofurahisha.

Mtalaamu wa masuala ya Tehama, Lazaro Njota, anasema kuna umuhimu wa kuweka mizania kati ya dunia ya kidijitali na maisha halisi, kinyume cha hapo ni kupungua kwa ujuzi wa kijamii.

“Matumizi ya teknolojia yanapochukua nafasi kupita kiasi hupunguza muda wa watu kuchangamana, ndiyo hayo ya wanafamilia wanakutana lakini kila mmoja ameinamia simu yake,” anasema na kushauri:

“Tuanze kulifanyia kazi kwa watoto, ikitokea anapewa nafasi ya kutumia teknolojia kwa kiasi na wakati huohuo akahimizwa kuchangamana na watu, hujenga uwezo mpana zaidi unaomsaidia kukabiliana na changamoto za kijamii na kiteknolojia.”

Anasema licha ya umuhimu wa teknolojia na vifaa vya mawasiliano, bado havina uwezo wa kuchukua nafasi ya binadamu linapokuja suala la mawasiliano ya kijamii.

Mila na desturi

Baadhi ya jamii za mikoa ya Kanda ya Kaskazini, huamini katika mikusanyiko hii ni muhimu kuchinja mnyama.

“Mtu akija nyumbani kipindi cha sikukuu akaondoka bila kuchinja, kuna wengine huamini mambo yake hayakai sawa. Kuchinja ni kama kufungua mwaka mpya kwa baraka,” anasema Atanasi Joseph, wa Rombo, mkoani Kilimanjaro.

Joseph anasema: “Kuchinja pia hutumika kama alama ya maridhiano. Pale ambapo migogoro imekuwapo kati ya ndugu au watoto wa familia, wazee hutumia fursa hii kuwakutanisha, kuwasikiliza na hatimaye kuhitimisha mzozo kwa tendo la kuchinja, ambalo huashiria mwisho wa ugomvi.”

Anasema mkusanyiko huo pia unaweza ukauita ‘mahakama ya familia’ kwani migogoro ikiwamo ya urithi au kutokuelewana katika hali yoyote ile hutafutiwa ufumbuzi.

“Mfano nina vijana watano. Wengine wanaweza kuwa hawaelewani. Wakikutana kipindi kama hiki na sisi wazazi tupo hai, ndipo tunamaliza mambo yao. Tunakaa nao chini tunazungumza, tunachinja na kuendelea na maisha kama kawaida,” anasema.

Damas Tesha, mkazi wa Rombo anasema: “Wazee wengine hutunza mbuzi kwa zaidi ya miaka miwili wakisubiri achinjwe katika sikukuu hizi kama sehemu ya sherehe ya kifamilia, kwetu mbuzi huyo huwa alama ya uvumilivu na maandalizi ya muda mrefu.”

Tesha anasema sikukuu za mwishoni mwa mwaka ni fursa kwa vijana kujifunza historia ya ukoo, kusikiliza simulizi za wazee na kuelewa wajibu wao katika kuendeleza mila.

“Unapokuja nyumbani, unakaa na wazee, unasikiliza hadithi za ukoo na kujifunza namna ya kuishi na watu. Hii inasaidia hata katika maisha ya sasa,” anasema.

Hali hii inazamwa na Emmanuel Kweka, mtaalamu wa saikolojia ya utamaduni, akisema ishara za kimila zina nguvu kubwa kuliko maneno peke yake.

Anasema tendo la kuchinja, kula pamoja na kushiriki shughuli za kifamilia hujenga hisia ya kufungua upya uhusiano, jambo linalosaidia pande zilizokuwa zinagombana kuanza ukurasa mpya bila kuendelea kubeba kinyongo.

“Katika saikolojia tunaita hii uponyaji wa kiibada. Hii husaidia akili ya binadamu kukubali mabadiliko. Unaposhuhudia tendo la pamoja linalotambuliwa na jamii nzima kama mwisho wa ugomvi, akili inakubali kuwa mgogoro umefungwa,” anasema.

Samson Andrew, mkazi wa wilayani Arumeru mkoani Arusha anasema mikusanyika inayofanyika inajenga umoja katika familia na kufanya jamii kuwa na maendeleo.

“Utaratibu huu umesaidia kufanyika kwa vikao vya familia, kuonyana pale watu wanapokuwa wamekosea au kufanya mambo ambayo hayaeleweki,” anasema na kuongeza:

“Kukutana mwisho wa mwaka kumesaidia vijana kujitambua kwani ikifika umri anatakiwa kuoa au kuolewa na hilo halijafanyika, kupitia vikao anaulizwa tatizo ni nini? Inasaidia wengi kuanzisha familia wakati sahihi ukiwadia.”

Kwa upande wa watoto, anasema huwasaidia kujua tamaduni za asili, vikiwamo vyakula na kuona mazingira wazazi wao wamekulia.

“Mimi huwa nawapeleka kila mwisho wa mwaka, wanajifunza shughuli za kijamii, ufugaji wa kuku na kumkamua ng’ombe maziwa. Mazingira mjini huwafanya wasijue tunapotoka na tamaduni zetu zilivyo,” anasema.

Utambulisho kwenye ukoo

Dementria Shirima, mkazi wa Moshi anasema katika kusanyiko nyumbani hufanyika utambulisho wa wana ukoo, wakiwamo watoto ambao hawakuwahi kufika nyumbani.

“Vijana ambao hawajawahi kuleta watoto nyumbani hutumia nafasi hii kuwatambulisha ndani ya familia. Baada ya utambulisho, wazee huchinja mnyama kama ishara ya kumkaribisha mjukuu nyumbani, kumpa baraka na kumtambua rasmi kama sehemu ya ukoo,” amesema.

Nsia Lema, mkazi wa jijini Arusha anasema: “Ndugu wa ukoo mzima tunakutana, tunajuana. Mkusanyiko huu unasaidia watu kufanya kazi kwa bidii, kwani unajua kila mwaka kuna kukutana na lazima uwe umeongeza kitu.”

Amesema kwa watoto waliozaliwa mijini, mikusanyiko hiyo kuwasaidia kujua mazingira tofauti.

“Wakati mwingine wakifunga shule tunawatanguliza huko waendelee kukaa na bibi na babu zao ili wajue mazingira tofauti na mjini,” anasema.

Mwanasaikolojia wa maendeleo ya mtoto, Rehema Lema, anasema hatua hiyo ina mchango mkubwa katika kujenga utambulisho na kujiamini kwa watoto.

Rehema anasema mtoto anapotambuliwa rasmi na ukoo, hupata hisia ya kukubalika na kuthaminiwa, hali inayomsaidia kuepuka matatizo ya kujitenga, aibu au hasira anapokua.

“Watoto wanaokosa utambulisho wa kifamilia mara nyingi hukua na maswali mengi kuhusu wao ni nani na wanatoka wapi. Mila hizi zinapofanyika, zinawapa msingi imara wa kisaikolojia na kuwajengea heshima kwa mizizi yao,” anasema.

Mkakati kiuchumi

Amos Akyoo, mkazi wa jijini Arusha anasema sikukuu hizi kwa familia yao ni fursa ya kuweka mipango ya pamoja ya kujiinua kiuchumi.

Anasema wameanzisha vikundi na umoja wa familia ambao wanaweka fedha kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

“Kwetu tuna utaratibu kila Krismasi tunakutana kijijini kwetu, tunajadiliana kila mmoja anaeleza mipango yake na mafanikio yake kwa ujumla,” anasema.

“Kupitia vikao hivyo tunajikuta kila mmoja anafanya kazi kwa bidii maana ikifika sikukuu unajua unapaswa kukutana na ndugu zako, hivyo ni lazima uwe umefanikiwa na kuongeza kitu,” anasema na kuongeza:

“Tumeanzisha mfuko, tukiwa na jambo la familia tunatoa hela kwenye mfuko wa pamoja, hii inasaidia kuongeza umoja wa familia na wakati mwingine tunainuana kiuchumi kupitia mfuko huo.”

Tiba ya kijamii

Mtaalamu wa saikolojia ya jamii, Neema Msuya, anasema mikusanyiko ya kifamilia ni tiba ya kijamii kwa kuwa huwakutanisha wanajamii pamoja.

Anasema kwa kukutana, kuzungumza kwa uwazi na kusikilizwa na wazee husaidia kupunguza msongo wa mawazo, hasira zilizofichika na maumivu ya muda mrefu yaliyokuwa hayajapatiwa suluhu.

“Watu wengi hubeba majeraha ya kihisia kwa muda mrefu, migogoro ya urithi, wivu wa kifamilia au kutokuelewana. Sikukuu zinapogeuzwa kuwa jukwaa la mazungumzo na maridhiano, zinasaidia ‘kusafisha’ akili na mioyo, jambo linalopunguza hatari ya msongo wa mawazo na hata magonjwa ya kisaikolojia,” anasema.

Hivyo ndivyo jamii inavyojipambanua kuelekea sikukuu za mwishoni na mwanzoni mwa mwaka; yapo mambo ya mila na mabadiliko, mikutano ya ana kwa ana na ya kidijitali, ya shangwe na tafakuri ya kimya kimya.

Ni kipindi kinachoonyesha wazi kuwa jamii si kitu kilichoganda, bali ni kiumbe hai kinachobadilika kulingana na nyakati.

Katika mabadiliko hayo, kila mmoja hutafuta mahali pake, iwe ni mezani nyumbani, kwenye kiti cha baa au nyuma ya mwanga wa skrini ya simu.

Imeandikwa na Janeth Joseph, Janeth Mushi na Elizabeth Edward

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *