Mchezaji wa zamani wa Simba, Kariakoo Lindi, na timu ya taifa ya vijana, Mnenge Suluja, amefariki dunia saa 5 usiku wa kuamkia Desemba 20, 2025 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Geita.

‎Kabla ya kifo hicho, Suluja alikuwa anaugua kwa muda mrefu ambapo wiki mbili zilizopita alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi, baada ya kupata nafuu alirejeshwa Geita, lakini juzi alizidiwa na kukimbizwa Hospitali ya Wilaya saa 5 asubuhi kwa ajili ya matibabu ndipo umauti ukamkuta wakati akitibiwa.

‎Suluja amewahi kuwa Katibu wa Chama cha Soka Wilaya ya Geita (GEDFA) tangu mwaka 2017 hadi 2025 alipokutana na adhabu ya kufungiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

‎Pia amewahi kuwa Katibu wa Chama cha Makocha Tanzania (TAFCA) Mkoa wa Geita, na Kamishna wa mechi za Ligi Kuu Bara na Championship, jukumu alilokuwa analifanya hadi kifo chake.

‎Akithibitisha taarifa hizo, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Geita (GEREFA), Salum Kulunge, amesema: ‎”Suluja alikuwa akisumbuliwa na maradhi mbalimbali, ambapo alilazwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kama wiki mbili, na baada ya kuonekana hali yake imeimarika akawa amerudishwa Geita, lakini juzi kwa ghafla tu ilionekana hali yake ilibadilika akawahishwa hospitali ya wilaya ambapo alipatiwa matibabu mpaka umauti ulipomkuta.

Kulunge amesema taratibu za mazishi zinaendelea kufanyika nyumbani kwa marehemu mjini Geita karibu na Shule ya Msingi Geita, ambapo kesho Jumapili atasafirishwa kwenda kwao wilayani Sengerema kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika kati ya Jumatatu na Jumanne wiki ijayo.

‎”Taratibu zilizopo ni kwamba leo Jumamosi pataendelea na misa tu hapo nyumbani kwake Geita, kesho Jumapili tutafanya maandalizi ya kuagwa ili kupelekwa nyumbani kwao Sengerema eneo la Nyantakubwa, taratibu za mazishi zitafanyika aidha Jumatatu ama Jumanne,” amesema Kulunge.

‎Akizungumzia mchango wa Suluja katika soka la mkoa wa Geita, Kulunge amesema wamempoteza mtu muhimu ambaye amekuwa ni kiunganishi kati ya vijana, makocha, timu za mkoa huo na wadau mbalimbali akiwa amelitumikia kwa takribani miaka 10.

‎”Tumepoteza mtu muhimu kwa sababu amekuwa mdau mkubwa kwa soka la mkoa wetu kuanzia soka la vijana, kusaidia mipango ya timu zetu ikiwemo Geita Gold, kuinua makocha, na hata kuongoza na kusimamia ligi za wilaya na za mkoa, kwahiyo alikuwa mtu muhimu kwa soka letu,” amesema.

‎Mdau wa soka mkoani Geita, Pius Kimisha, amesema amemfahamu Suluja kwa muda mrefu tangu anacheza soka mpaka alipostaafu na kuingia kwenye uongozi, ambapo siku za hivi karibuni alikuwa anaugua mara kwa mara.

‎”Alikuwa anaumwa muda mrefu afya kidogo iliyumba, mwezi huu ameugua akalazwa huku (Geita) baadae wakampeleka Bugando, wamemtoa wiki iliyokwisha tu hospitalini, sasa hivi hana wiki toka wamemtoa hospitali alikuwa anaanza kupata nafuu,” amesema Kimisha na kuongeza;

‎”Lakini toka amerudi nyumbani alikuwa na changamoto ya kutapika kila anachokula. Jana walichukua hatua ya kumpeleka hospitali kufikia hiyo saa 5 usiku akafariki, amelazwa pale kwa siku mbili.”

‎Kimisha ambaye alikuwa Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Geita (GEREFA) kwa miaka 10, amesema alimpokea Suluja kwenye uongozi kuanzia mwaka 2017 aliposhika nafasi ya Katibu wa GEDFA na baadae kuongoza katika nyadhifa mbalimbali.

‎”Baada ya kustaafu soka alikuja kuingia kwenye uongozi, tumefanya naye kazi akiwa Katibu wa Chama cha Mpira Wilaya, tumefanya naye miaka isiyopungua tisa, alikuwa mtu mwema, wa kujituma, na mpira alikuwa anaujua,” amesema Kimisha.

‎Ameongeza: “Pia ni kocha na amewahi kuwa Katibu wa Makocha Tanzania (TAFCA) mkoa wa Geita, kwa hiyo ametumika sana kwenye soka la mkoa wetu, nafikiri ameingia kwenye uongozi tangu mwaka 2017, alinikuta mimi na amefanya kazi muda mrefu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *