
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja janaDesemba 19, 2025 limepitisha azimio namba 2808 (2025), ambalo linaamua kuongeza hadi tarehe 20 Desemba 2026 muda wa kazi wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO), na kwa hali ya kipekee, wa brigedi yake ya kukabiliana mashambulizi.
Kupitia azimio lililowasilishwa na Ufaransa, Baraza limeamua kwamba MONUSCO itaendelea kuwa na idadi ya juu iliyoidhinishwa ya wanajeshi 11,500, waangalizi wa kijeshi na maafisa wa makao makuu 600, askari polisi 443, na wafanyakazi1,270 wa vitengo vya polisi vilivyoundwa.
Pia linaamua kwamba vipaumbele vya kimkakati vya MONUSCO ni kuchangia: ulinzi wa raia katika eneo lake la upelekwaji; utekelezaji wa malengo yaliyowekwa na azimio 2773 (2025); na utulivu pamoja na uimarishaji wa taasisi za kitaifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Zaidi ya hayo, Baraza linaidhinisha MONUSCO kusaidia utekelezaji wa sitisho la kudumu la mapigano kwa mujibu wa azimio 2773 (2025).
Azimio hilo pia limeangazia kile linachokiita “kuharibika kwa kasi kwa hali ya usalama na kibinadamu” mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kufuatia mashambulizi ya kundi la waasi M23 (Mouvement du 23 Mars) katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, “kwa msaada wa moja kwa moja na ushiriki wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda.”
Aidha, azimio hilo lilikemea vikali kutekwa kwa mji wa Uvira, mji wa kimkakati ulioko Kivu Kusini kandokando ya Ziwa Tanganyika, likionya kuwa hatua hiyo inaweza kuhatarisha uthabiti wa eneo pana la Maziwa Makuu. Eneo la Mashariki mwa DRC lina utajiri mkubwa wa madini na inaaminika madola ya magharibi yanachochea mapigano katika eneo hilo kwa lengo la kupora madini hayo ambayo ni muhimu katika teknolojia za kisasa.