Morogoro. Ofisi ya Taifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (NAOT), imevitaja vyombo vya habari nchini kama washirika kimkakati katika kuibua mijadala ya uwajibikaji wa fedha za umma.

Mkaguzi Mkuu wa Nje (CEA), Baraka Mfugale, ametoa kauli hiyo jana Desemba 19, 2025, katika mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari mjini hapa.

Amesema kazi ya wanahabari ni kutoa uhai kwa ripoti za ukaguzi kwa kuzifikisha kwa wananchi, jambo linalosaidia ripoti hizo kutobaki kama nyaraka za ofisini pekee.

Mfugale ameongeza kuwa Ofisi ya mkaguzi itaendelea kuboresha mifumo yake ya mawasiliano, ili kuwajengea wananchi uelewa mpana kuhusu mamlaka na mipaka ya ofisi hiyo katika usimamizi wa mali za umma.

 “Tunategemea vyombo vya habari kufafanua ripoti hizi kwa lugha rahisi, kuchambua hoja zake na kuibua maswali yatakayosaidia kuboresha usimamizi wa rasilimali za umma,” amesema.

Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika mafunzo ya ukaguzi kwa vyombo vya habari iliyofanyika mkoani Morogoro. Picha na Juma Mtanda.

Mfugale amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea waandishi wa habari uwezo wa kusoma na kuchambua ripoti za ukaguzi kwa kina, kutafsiri takwimu na kuelewa mapendekezo ya ukaguzi ili kusaidia taasisi za serikali, Bunge na wadau wengine kuchukua hatua stahiki.

Kwa mujibu wa Mfugale, hadi kufikia Juni 2025, Ofisi yake imetoa mafunzo ya uelewa wa ukaguzi kwa waandishi wa habari, asasi za kiraia na wadau wengine katika mikoa 21 nchini, yakihusisha washiriki zaidi ya 630.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini ofisi hiyo , Focus Mauki, amesema mada zilizofundishwa ni pamoja na ukaguzi wa serikali za mitaa, aina na mbinu za ukaguzi, pamoja na majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa mujibu wa Katiba.

Naye Mkaguzi wa Nje kutoka Divisheni ya Serikali za Mitaa, Mary Dibogo, amesema ukaguzi wa hesabu za serikali za mitaa unaongozwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hususan Ibara ya 143, inayobainisha mamlaka ya Ofisi ya Mkaguzi  katika kusimamia matumizi ya rasilimali za umma.

Akizungumza kwa niaba ya wanahabari, Katibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Morogoro, Lilian Lucas, amesema mafunzo hayo yamewasaidia waandishi wa habari kuelewa namna ya kutumia ripoti za ukaguzi kama nyenzo ya kuandika habari za uwajibikaji na uchunguzi.

Lilian amesema kupitia mafunzo hayo, waandishi wa habari watakuwa na uwezo zaidi wa kuchambua taarifa nzito za kitaalamu na kuziwasilisha kwa jamii kwa lugha rahisi, hatua itakayosaidia wananchi kuwa na uelewa mpana baada ya ripoti za ukaguzi katika ngazi mbalimbali kutolewa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *