Dar es Salaam. Ni wazi kuwa uhusiano wa Jux na mkewe Priscilla kutokea Nigeria umekuza kwa kiwango kikubwa chapa zao tena ndani ya muda mfupi na kufungua fursa za kikazi na hata kibiashara kwa pande zote mbili.
Kwa sasa ni rahisi kwa Jux kufanya show Nigeria na hata kushirikiana na wasanii wa nchi hiyo huku Priscilla akipata dili kadhaa za ubalozi kutokea Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Mathalani hapo juzi Jux alitumbuiza huko Lagos katika tamasha la Detty huku akisindikizwa na Diamond Platnumz ambaye wameshirikiana katika nyimbo tatu, Sugua (2019), Enjoy (2023) na Ololufe Mi (2024).
Hii sio show ya kwanza kwa Jux kufanya Nigeria, tangu mwishoni mwa Octoba amekuwa na shughuli nyingi za kisanaa nchini humu na kupata mapokezi mazuri na mara zote amekuwa akiongozana na mkewe.
Miaka mitatu nyuma Jux hakuwa na ushawishi huo katika kiwanda cha burudani Nigeria lakini sasa milango kwa upande wake imefunguka, naye anatumia fursa hiyo ipasavyo.
Hayo yote yanafanyika kwa sababu Jux na Priscilla wamefanikiwa kubadilishana mashabiki na nguvu ya ushawishi waliyonayo ndani ya nchi zao kupitia sanaa yao ya muziki, filamu na mitindo.
Utakumbuka Februari ndipo Jux alifunga ndoa na Priscilla ambaye ni binti wa Iyabo Ojo, mmoja wa waigizaji wakongwe huko Nollywood akiwa amecheza filamu zaidi ya 150 tangu miaka ya 1990.
Wakati wanajiandaa kufanya harusi yao ndipo Jux alitoa wimbo wake ‘God Design’ uliokuja kujumuishwa katika Extended Playlist (EP) yake ya kwanza, A Day To Remember (2025) yenye nyimbo saba.
Wimbo huo uliotayarishwa na Foxx Made It, Jux amemshirikisha rapa mwenye mashabiki wengi Nigeria, Phyno ambaye awali alishafanya kazi na Rayvanny, mwanzilishi wa Next Level Music (NLM).
Huu ulikuwa mkakati wa kuendelea kujiimarisha katika soko la Nigeria kama mwanamuziki mwenye kiu ya kufika mbali baada ya kupokelewa vizuri kama shemeji yao baada ya kuzama penzini na Priscilla.
Jux na Priscilla walianza kuonekana pamoja hadharani Julai 2024 ikiwa ni miezi kadhaa tangu mwanamuziki huyo kuachana na aliyekuwa mpenzi wake, Karen Bujulu.
Wakati wanatambulisha uhusiano wao, Priscilla a.k.a Priscy alikuwa na wafuasi (followers) milioni 2.8 katika ukurasa wake wa Instagram ila kwa sasa wameongezeka hadi kufikia milioni 4.5.
Wengi waliongezeka hapo ni mashabiki wa Jux, hii sio sifa tu ya bure bali ina maana kubwa kwa Priscilla akiwa kama mshawishi wa chapa mtandaoni (influencer), kazi ambayo imemkutanisha na chapa mbalimbali.
Kuongezeka kwa namba zake mtandaoni ambapo kwa sehemu kumechangiwa na uhusiano wake na Jux, ni wazi kunampatia fursa ya kusaini dili nyingi za matangazo akiwa kama balozi wa huduma au bidhaa fulani.
Tayari alishapewa dili kadhaa za ubalozi kutokea hapa nchini, kitu ambacho ingekuwa ni vigumu kukipata miaka mitatu nyuma ambapo hakuwa na uhusiano na Jux.
Hapo awali, miongoni mwa chapa alizofanya nazo kazi ni kampuni ya cryptocurrency ChiJ14Exchange, kampuni ya utengenezaji wa filamu ya Viskit, chapa ya vipodozi Hegai and Esther na kampuni ya Itel Nigeria.
Pia chapa za urembo na mitindo kama House Of Sweeter Things, Sunglasses and Moore, Cassie Hair, Top Posh Collections, Beautiful Body Nigeria, St. Nalex Wears, Gattyz Makeovers, DMC Luxury, Lady Bug Cosmetics n.k.
Akiwa kama mwanzilishi wa chapa yake ya mavazi, Priscy Closet, Priscilla ameshuhudia mabadiliko makubwa katika kazi yake tangu amekuwa na Jux, na ni wazi hata dau lake katika mikataba limeongezeka.
“Anatengeneza fedha kwa hiyo inanipunguzia msongo wa mawazo. Niliruhusiwa kufanya nilichotaka, hivyo nilitarajia hilo pia kwa watoto wangu,” alisema mama yake, Priscilla, Ojo wakati ameanza kujihusisha na mitandao.
Kabla ya kuanza kazi ya ushawishi wa chapa mtandaoni, Priscilla alianza kuigiza katika filamu za Nigeria na nyingi zikitayarishwa na mama yake.
Alipokuwa na umri wa miaka 14, Priscilla aliteuliwa kuwania Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike katika Tamasha la Filamu Nigeria 2015 baada ya kufanya vizuri katika filamu ya Beyond Disability (2014)