Rais Yoweri Museveni wa Uganda amewaonya wale wanaopanga kuandamana na kueleza kwamba, kuna risasi za kutosha kwa ajili ya kukabiliana nao.

Rais Museveni alitoa matamshi hayo wakati akijibu swali la mwanahabari katika moja ya vikao vya jioni vya kampeni zake. Swali hilo lilihusu mwito wa mara kwa mara wa mpinzani wake mkuu, Robert Kyagulanyi, anayejulikana kama Bobi Wine, anayewahimiza wapigakura kubaki kwenye vituo vya kupigia kura ili kuhakikisha kura zao haziibiwi.

Akijibu, rais Museveni ambaye ni mgombea wa chama tawala cha NRM, alisema kuwa askari wa usalama wako tayari kukabiliana na vurugu zozote, akitaja idadi ya risasi walizonazo kama ishara ya nguvu ya dola. “Nimekuwa nikimsikia Kyagulanyi akisema askari ni wachache na wanaoweza kufanya vurugu ni wengi. Msimsikilize, kwa sababu kila askari ana risasi 120. Mkisema wanaofanya vurugu ni wengi, walingenisheni na idadi ya risasi za askari,” alisema Museveni.

Kauli hiyo imeibua hofu na wasiwasi miongoni mwa wananchi wengi, huku baadhi wakisema matamshi hayo yanaweza kuwakatisha tamaa raia kujitokeza kupiga kura. Wengine wameeleza kuwa amani na uthabiti wa taifa haviwezi kudumishwa kwa vitisho vya silaha.

Baadhi ya wananchi wamekosoa mtazamo huo wakisema kuwa historia ya dunia inaonyesha kuwa nguvu za kijeshi haziwezi kuzima sauti ya watu kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, mgombea wa chama kikuu cha upinzani cha National Unity Platform (NUP), Robert Kyagulanyi, amemshtumu vikali rais Museveni kwa kauli hiyo, akisema ni ya kutisha na inayokiuka misingi ya haki za binadamu.

Kyagulanyi aliwahimiza polisi na wanajeshi kutokubali kutumiwa kuwaua wananchi wenzao wanaotekeleza haki zao za kikatiba wakati wa uchaguzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *