KLABU ya Namungo ‘Wauaji wa Kusini’, imeanza mazungumzo ya kumsajili beki wa kati wa KMC, Salum Athuman ‘Stopper’, kwa ajili ya kwenda kuchukua nafasi ya Abdallah Mfuko, anayedaiwa yuko katika harakati za kutua Mbeya City.

Mfuko aliyebakisha mkataba wa miezi sita, inadaiwa anataka kuachana na timu hiyo wakati dirisha dogo litakapofunguliwa Januari Mosi 2026, kwa lengo la kuungana na Kocha Mecky Maxime, aliyewahi kufanya naye kazi katika kikosi cha Kagera Sugar.

Wakati dili la Mfuko likiendelea kufukuta, mabosi wa Namungo wameanza mazungumzo ya kumpata Stopper ambaye mkataba wake na KMC umebakia miezi sita, jambo linaloweza kurahisisha uhamisho huo dirisha hili.

Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Namungo, zililiambia Mwanaspoti Stopper ni miongoni mwa machaguo ya wachezaji wa beki wa kati wanaowafuatilia kutokana na uwezo wake tangu ajiunge na kikosi hicho, ingawa hadi sasa hakuna makubaliano rasmi.

Beki huyo ambaye ni zao la timu ya vijana ya Simba, amekuwa na kiwango bora na KMC aliyojiunga nayo kwa mara ya kwanza Juni 30, 2024, akitokea KVZ ya visiwani Zanzibar na alisaini mkataba wa miaka miwili unaoisha msimu huu.

Nyota huyo amewahi kupita katika timu ya Fountain Gate ikiwa ni sehemu ya makuzi katika safari yake na baadaye alijiunga na JKT Tanzania, Mbeya Kwanza, kisha kutimkia Zanzibar alikoonyesha kiwango bora kilichoivutia KMC kumsajili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *