Dar es Salaam. Mwaka 2025 umebeba simanzi katika historia ya siasa za Tanzania, baada ya Taifa kupoteza viongozi na wanasiasa mashuhuri waliowahi kulitumikia kwa muda mrefu, ikiwamo kutoa mchango katika maendeleo ya nchi.

Katika nyakati tofauti ndani ya mwaka huu, Watanzania walikumbwa na huzuni kufuatia vifo vya viongozi hao, akiwemo Cleopa Msuya, Job Ndugai, Profesa Philemon Sarungi, Mateo Qares, Nicodemus Banduka, Abbas Mwinyi na majuzi tu Jenista Mhagama.

Viongozi hawa wataendelea kukumbukwa kwa mchango wao katika siasa na utumishi wa umma.

Cleopa Msuya

Waziri Mkuu mstaafu Cleopa Msuya (94) alifariki dunia Mei 7, 2025 na alizikwa kijijini kwake Usangi mkoani Kilimanjaro.

Msuya aliwahi kuwa waziri mkuu wa Tanzania mara mbili kwa marais tofauti. Mara ya kwanza alikuwa waziri mkuu kuanzia 1980–1983 chini ya Mwalimu Nyerere.

Mara ya pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi alipoteuliwa pia kuwa makamu wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wadhifa uliounganishwa na nafasi ya waziri mkuu kuanzia mwaka 1994 hadi 1995.

Pia, aliwahi kuteuliwa kuwa waziri wa Fedha mwaka 1972, na baadaye waziri wa Viwanda mwaka 1975.

Msuya alikuwa na mchango mkubwa hususan katika nyanja za ufadhili na uundaji wa sera za uchumi, hasa katika kipindi kigumu cha changamoto za kiuchumi kilichofuata enzi ya ujamaa.

Katika kipindi hicho, alionyesha uongozi wa hekima na uzoefu mkubwa katika kusimamia mabadiliko ya kiuchumi ya Taifa.

Alifanya kazi kwa karibu na mashirika ya kimataifa, yakiwemo Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, katika kutafuta na kutekeleza mipango ya kurejesha ustawi wa uchumi pamoja na kuanzisha na kusimamia marekebisho muhimu ya sera za kiuchumi.

Nicodemus Banduka

Nicodemus Banduka mbali na kazi ya ukuu wa mkoa kwenye mikoa kadhaa, pia alikuwa mmoja wa viongozi waliotoa mchango wa kihistoria katika safari ya kisiasa ya Tanzania, hususan katika mchakato wa kuundwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Banduka, aliyefariki dunia Februari 7, 2025, enzi za uhai wake miongoni mwa majukumu yake muhimu na ya kihistoria ni uteuzi wake mwaka 1976 kuwa mmoja wa wajumbe 20 wa Tume Maalumu iliyoanzishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Tanu.

Tume hiyo ilikabidhiwa dhamana ya kusimamia na kuratibu mchakato wa kuunganisha vyama vya Tanu na Afro-Shirazi Party (ASP), jukumu lililohitaji busara, maridhiano na maamuzi ya kina, na ambalo hatimaye liliweka msingi wa kuundwa kwa CCM mwaka 1977.

Banduka na wenzake 10 kutoka Tanu (Tanzania Bara) na wengine 10 kutoka ASP (Zanzibar) walipewa kazi ya kupitia na kupendekeza muundo wa chama kipya, ikiwemo jina la chama, bendera, katiba, itikadi, rangi, nembo ya chama na misingi ya uendeshaji na uongozi wa chama kitakachozaliwa kutokana na muungano huo.

Profesa Sarungi

Katika orodha hiyo, yumo Profesa Sarungi (89), ambaye alikuwa daktari bingwa wa upasuaji na tiba ya mifupa, aliyefariki dunia Machi 5, 2025, jijini Dar es Salaam.

Mbali na utaalamu wake katika sekta ya afya, Profesa Sarungi aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za uwaziri ikiwemo waziri wa Afya, waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na waziri wa Elimu.

Mwanasiasa huyo, atakumbukwa zaidi kwa maono yake ya kuanzishwa kwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), ambayo hadi leo inaendelea kuokoa maisha ya Watanzania wengi.

Pia, Profesa Sarungi anakumbukwa kwa kuweka ‘hospitali pori’ au kambi ya matibabu wakati wa ajali ya treni iliyotokea Juni 24, 2002 eneo la Msagali na Igandu, mkoani Dodoma.

Wakati ajali hiyo inatokea, Profesa Sarungi alikuwa mbunge wa Rorya na pia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Badala ya kubaki ofisini akitoa maelekezo ya kiutawala, Profesa Sarungi alifika eneo la ajali mapema akiwa na timu ya madaktari wa kijeshi na raia.

Alianzisha kambi ya dharura  papo hapo eneo la tukio  ili kuwapa huduma ya kwanza majeruhi kabla ya kuwahamishia Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

Pia, Profesa Sarungi, akiwa amevaa mavazi yake ya kitabibu katikati ya vumbi na mazingira ya porini, alisaidia kufanya upasuaji na kutoa huduma za kitaalamu kuokoa maisha ya watu waliokuwa wamenasa kwenye mabehewa.

Alitumia nafasi yake kama Waziri wa Ulinzi kuratibu helikopta za jeshi na magari ya kubeba wagonjwa kusafirisha majeruhi na miili ya marehemu.

Mateo Qares

Mateo Qares ni mwanasiasa aliyewahi kuwa mbunge, waziri na mkuu wa mikoa mbalimbali nchini, ambaye alifariki dunia Julai 9, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alipokuwa akipatiwa matibabu.

Qares anakumbukwa kwa kuwamo kwenye kundi la wabunge 55 au kundi la G-55 mwanzoni mwa miaka 1990, wakati nchi ikiwa kwenye mfumo wa chama cha siasa.

Kundi hilo iliyoasisiwa na Mbunge wa Chunya, Njelu Kasaka (marehemu), liliunganisha wabunge hao wakidai kuwe na serikali tatu: Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Muungano.

Sababu za madai yao zilichochewa na matukio mawili makubwa ya kisiasa mwaka 1992/1993 ambayo ni Zanzibar ilijiunga na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kama nchi huru, jambo ambalo lilipingwa na Serikali ya Muungano na kuonekana kuwa ni ukiukwaji wa Katiba (kwani mambo ya nje ni ya Muungano).

Pia, wabunge wa G-55 walihisi kuwa Tanganyika “imefungwa” ndani ya koti la Muungano huku Zanzibar ikiwa na serikali yake, bendera yake, na wimbo wake wa Taifa. Walidai kuwa Tanganyika inapoteza utambulisho wake na inabeba mzigo mkubwa wa gharama za Muungano bila kuwa na mamlaka ya kijitawala.

Hoja ya G-55 ilifanikiwa kupita bungeni kwa kauli moja Agosti 1993. Hata hivyo, hali ilibadilika baada ya Mwalimu Nyerere kuingilia kati na kuipinga akidai kuwa kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika ni mwanzo wa kuvunjika kwa Muungano.

Pia, Mwalimu Nyerere aliandika kitabu maarufu cha “Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania” (1994) kuwashambulia na kukosoa uongozi wa Rais Ali Hassan Mwinyi kwa kuruhusu hoja hiyo kupita.

Kutokana na shinikizo la Nyerere, CCM ililazimika “kuirudisha nyuma” hoja hiyo, na serikali ya Serikali mbili ikaendelea kuwepo.

Job Ndugai

Ndugai aliyekuwa mbunge wa muda mrefu wa Kongwa, alifariki Agosti 6, 2025 mkoani Dodoma. Mwanasiasa huyo alifariki dunia katika ya mchakato wa kura za maoni za ndani za kuwapa wagombea watakaopeperusha bendera ya CCM.

Ndugai atakumbukwa kwa kuacha alama kama kiongozi aliyebeba majukumu ya Bunge kwa uzito mkubwa. Uongozi wake ulitoa somo kuhusu uwajibikaji wa viongozi, nafasi ya Bunge huku wapinzani wakikumbana na mkono wa chuma.

Wameacha pengo

Baadhi ya wachambuzi wa siasa, waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wamesema vifo vya wanasiasa hao vimeacha pengo kubwa kutokana kazi kubwa walioifanya wakati wakitumikia nyadhifa zao ndani ya chama na Serikali.

Mchambuzi wa siasa na jamii, Seif Nassor amesema kifo kinapotokea kinaacha pengo, ndivyo ilivyotokea kwa wanasiasa hao ambao kila mmoja ana umuhimu wake kuanzia katika jamii na familia zao.

Akitolea mfano msiba wa karibuni kabisa, anasema: “Mhagama alikuwa mwanamke jasiri, alikuwa ‘active’ tangu akiwa kijana na mpambanaji, hadi kufikia ngazi ya kuwa mwenyekiti wa Bunge. Alikuwa mtetezi wa wanawake wenzake, ni pengo kubwa,” anasema Nassor.

Nassor anasisitiza kuwa kifo cha Mhagama ni pengo kubwa hata wanawake wenzake waliopo kwenye siasa na wabunge wanafahamu hilo.

Kuhusu Profesa Sarungi, Nassor anadai hadi sasa hajawahi kutokea bingwa wa mifupa kama Sarungi, alikuwa mtu muhimu aliyejitolea kuwasaidia Watanzania akitolea mfano ajali ya treni iliyotokea Dodoma.

Katika ajali hiyo, Nassor anasema Profesa Sarungi aliuweka uwaziri pembeni akajumuika na madaktari wenzake, kutoa msaada kwa majeruhi.

“Tukubaliane ni pengo kuwa lililoachwa na Profesa Sarungi, hadi sasa hajatokea mwenyewe uwezo mkubwa kama yeye. Hata alipostaafu alibaki kuwa mshauri wa madaktari wenzake,” anaeleza Nassor.

Kwa mujibu wa Nassor, Ndugai atakumbukwa namna alivyofuata nyayo za maspika wenzake waliomtanguliwa kuongoza mhimili wa Bunge kwa nyakati tofauti.

“Alifanya kazi nzuri na alijitahidi sana katika utekelezaji wa majukumu yake, ameacha pengo kubwa,” anasema Nassor.

Kwa upande wake Kiama Mwaimu, mchambuzi mwinvine wa siasa, anasema kifo ni jambo lisiloepukika kwa binadamu, lakini kuna watu wakifariki uhuzunisha na kusikitisha kwa sabbau wanasaidia kutoa mawazo, fikra na ushauri wa kijamii au kitaifa.

“Kwa hawa waliotutangulia mbele ya haki, tutawakumbuka kwa maisha yao waliokuwa wakihudumu au kufanya kazi ya kulitumikia Taifa, tuliobaki tuwaombee kwa Mungu,” anasema.

Mwaimu anasema wote waliotangulia mbele ya haki, walikuwa watu wema katika jamii, na kama kulikuwa na mapungufu basi ya kibinadamu, kwa sababu hakuna aliye mkamilifu chini ya jua.

“Qares ni mtu niliyebahatika kuonana naye, alikuwa mkweli na mchapakazi, ukitofautiana naye anakueleza ukweli,” anasema Mwaimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *