Katika hatua ya kiupendeleo ya kuuunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel, Marekani imewawekea vikwazo majaji wawili wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC.
Alkhamisi ya tarehe 18 Desemba, Marekani ilitangaza kuwawekea vikwazo majaji wawili wa Mahakama ya ICC, baada ya majaji hao kutupilia mbali rufaa ya Israel ya kutaka faili la uchunguzi wa jinai za kivita zilizofanywa na jeshi la utawala huo wa kizayuni huko Ghaza lifungwe.
Majaji ambao wamelengwa na vikwazo vipya vya Marekani ni Gocha Lordkipanidze, ambaye ni waziri wa zamani wa sheria wa Georgia, na Erdenebalsuren Damdin, jaji kutoka Mongolia.
Kwa mujibu wa vikwazo hivyo, majaji hao hawataruhusiwa kuingia Marekani; na mali zao zilizoko nchini humo zitazuiliwa na miamala yoyote ya kifedha watakayofanya itasimamishwa. Lordkipanidze aliwahi huko nyuma kufundisha kama mhadhiri mwalikwa katika Chuo Kikuu cha Columbia huko New York.
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, yenye makao yake makuu The Hague, Uholanzi, imetoa mjibizo kupitia taarifa rasmi ikisema “inapinga vikali” vikwazo hivyo vipya vilivyowekwa na Marekani dhidi ya mahakimu wake. Mahakama hiyo imeeleza katika taarifa hiyo kwamba, hatua hiyo ya Washington ni “hujuma ya dhahiri kabisa dhidi ya uhuru wa taasisi ya mahakama isiyoegemea upande wowote.”
Hata hivyo, utawala wa kizayuni wa Israel umekaribisha hatua hiyo ya Marekani. Waziri wa mambo ya nje wa utawala huo Gideon Saar amempongeza mwenzake wa Marekani kupitia ujumbe alioweka kwenye mtandao wa kijamii wa X, akiitaja hatua hiyo ya Washington kuwa ni “msimamo wa bayana na wa kimaadili.”
Hatua hiyo ya Washington imeifanya idadi ya majaji wa ICC waliowekewa vikwazo na serikali ya Trump kufikia wanane. Halikadhalika, waendesha mashtaka wasiopungua watatu, akiwemo Karim Khan, ambaye ni mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo, nao pia wako kwenye orodha ya waliowekewa vikwazo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, ambaye alitangaza hapo kabla kuwawekea vikwazo majaji na waendesha mashtaka wengine waliohusika katika kesi dhidi ya Israel ametamka bayana kuwa, vikwazo hivyo vipya vina uhusiano wa moja kwa moja na hukumu ya uamuzi iliyotolewa na ICC Jumatatu ya Desemba 15, ambapo majaji hao wawili walikubaliana na rai ya walio wengi na kuidhinisha hati zilizotolewa na mahakama hiyo ya kimataifa za kukamatwa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wa zamani wa vita Yoav Gallant. Rubio amedai kwamba ICC imeendelea kujihusisha na shughuli za kisiasa dhidi ya Israel na kuanzisha mfano hatarishi kwa nchi zote. Sambamba na kuunga mkono uhalifu na jinai za utawala wa Israel, Rubio ameongezea kwa kusema: “hatutavumilia ICC kutumia vibaya nafasi yake na kuwalenga Wamarekani na Waisraeli kwa namna isiyo sahihi.” Bila kujali hadhi ya kisheria ya ICC, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ametoa onyo kwa kusema: “tutaendelea kutoa mijibizo inayostahiki na yenye matokeo yanayoonekana kwa hatua na ukiukaji unaofanywa na ICC.”
Hukumu ya uamuzi huo iliyotolewa Jumatatu na yenye kurasa 44 imethibitisha na kutilia mkazo uamuzi wa kuendelea kuchunguza tuhuma za jinai za kivita zilizofanywa na Israel katika Ukanda wa Ghaza. Netanyahu na Gallant wote wawili wanakabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu kutokana na mashambulio ya kinyama ya mtawalia yaliyofanywa na utawala wa kizayuni katika maeneo ya Palestina.
Nukta moja yenye umuhimu hapa ni kwamba, vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai vimekabiliwa na mijibizo hasi ya baadhi ya nchi za Ulaya, ikiwa ni pamoja na Ufaransa, Uhispania, Uholanzi na Denmark.
Vikwazo hivyo vinaweza kutafsiriwa kama moja ya vielelezo muhimu zaidi vya makabiliano kati ya Marekani na taasisi za kimataifa. Hatua hiyo haionekani tu kama shinikizo la kisiasa dhidi ya taasisi huru, lakini pia inaonyesha kwa uwazi namna Washington inavyopingana na kukabiliana na sheria na kanuni za kimataifa. Hatua hiyo ya serikali ya Marekani inaweza kuchambuliwa kwa kuzingatia misingi mikuu kadhaa.
Msingi wa kwanza ni kwamba, Marekani siku zote imekuwa ikionyesha kuguswa na kushughulishwa sana na ustahiki na uhalali wa kisheria wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai. Nchi hiyo si mwanachama wa Mkataba wa Roma, na tangu mwanzo imekuwa ikifanya juu chini kuhakikisha vikosi vyake vya kijeshi na maafisa wake wa kisiasa wanakuwa na kinga ya kutoweza kufuatiliwa kisheria na Mahakama ya ICC. Kwa mtazamo wa Washington, uchunguzi au hatua ya aina yoyote ya ICC dhidi ya raia wake au wa waitifaki wake wa karibu, hasahasa unaohusiana na vita na operesheni za kijeshi, ni tishio la moja kwa moja kwa mamlaka ya taifa ya kujitawala ya Marekani. Kwa hivyo, vikwazo vinaweza kuchukuliwa kama mjibizo wa kuizuia Mahakama ya ICC isije kufuatilia kesi ambazo zinaweza kupelekea kuwajibishwa maafisa wa Marekani.
Msingi wa pili ni kuwa, hatua hiyo ina chimbuko katika sera za nje za Marekani, ambazo mara nyingi hutekelezwa kwa msingi wa kuionyesha nchi hiyo kuwa iko juu ya mataifa mengine yote na isiyoweza kuwekewa mipaka na sheria za kimataifa. Washington huwa inazikubali taasisi za kimataifa pale zinapofanya kazi kuendana na maslahi yake, lakini wakati taasisi hizo zinapofanya kazi kwa uhuru na nje ya mfumo wa sera za Marekani, hukabiliwa na mashinikizo na vikwazo vya nchi hiyo. Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ambayo ni taasisi inayofanya kazi kwa uhuru inao uwezo wa kuchunguza kesi zinazokinzana na sera za Marekani, kama vile kadhia ya Palestina au Afghanistan. Kufanya kazi huko kwa uhuru ndio sababu kuu ya hatua kali zinazochukuliwa na Washington dhidi ya taasisi hiyo.

Lakini msingi wa tatu ni kwamba, vikwazo hivyo vinafikisha pia ujumbe wazi wa kisiasa. Marekani inataka kuzionyesha nchi zingine na taasisi za kimataifa kwamba hatua yoyote iliyo dhidi ya maslahi yake hitaachwa bila kujibiwa. Ujumbe huo hautolewi kwa Mahakama ya ICC pekee, bali pia kwa taasisi zingine, kuzitaka zijiepushe na kujiingiza kwenye kesi na kadhia ambazo zinaweza kuwa na madhara kwa Washington. Kwa kweli, vikwazo hivyo dhidi ya majaji wawili wa ICC ni sehemu ya mkakati wa Marekani wa kujiwekea ngao ya kutoandamwa katika uga wa sheria za kimataifa.
Kusema kweli, vikwazo vipya ambavyo Marekani imeiwekea Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ni hujuma ya dhahiri kabisa dhidi ya sheria na taasisi za kimataifa. Hatua hiyo inaonyesha kwamba Marekani iko tayari kukiuka hata kanuni za msingi kabisa za haki na uadilifu wa kimataifa ili kujiwekea kinga na kulinda maslahi yake. Mwelekeo kama huu sio tu unadhoofisha itibari ya ICC, lakini pia unatoa changamoto kubwa ya uasi dhidi ya nidhamu ya kisheria za kimataifa. /