
Rais wa Ghana, John Dramani Mahama, amekutana na kuzungumza wajumbe wa kimataifa, lengo likiwa ni kutafuta fidia ya utumwa na ukoloni wa Wazungu katika maeneo mbalimbali ya dunia hasa barani Afrika.
Wajumbe hao wamemsihi Rais wa Ghana kuwakusanya viongozi wengine wa Afrika ili kudumisha “ujasiri na kuunga mkono harakati hiyo inayopiga hatua ya kudai fidia ya vitendo vya utumwa na ukoloni duniani.”
Ujumbe huo wa kimataifa uliowajumuisha wataalamu kutoka Afrika, Caribbean, Ulaya Latini Amerika na Marekani waliwasilisha kwa Rais Mahama hatua za kipaumbele kulingana na ajenda ya ulipaji fidia ya Umoja wa Afrika (AU).
Haya yanajiri Ghana ikiwa mwenyeji wa Mkutano wa Diaspora 2025 katika mji mkuu wa nchi hiyo Accra, huku ukatili wa utumwa na jitihada za kulipwa fidia zikiwa mojawapo ya masuala muhimu yaliyogubika mkutano huo.
Itakumbukwa kuwa, Mwezi Februari mwaka huu Umoja wa Afrika ulianzisha harakati ya kuasisi “dira ya pamoja” kuhusu fidia itakavyotolewa hadi kukiri rasmi makosa yaliyofanywa na nchi za Magharibi kuelekea mageuzi ya sera.
Takriban Waafrika milioni 12.5 walitekwa nyara na kusafirishwa kwa nguvu na Wazungu, kisha kuuzwa utumwani kuanzia karne ya 15 hadi 19.
Nchi zilizoathirika na utumwa duniani likiwemo bara la Afrika, zinaendelea kupaza sauti zao zikidai kulipwa fidia. Hata hivyo viongozi wa nchi za Ulaya wamekataa hata kujadili jambo hilo.
Ghana imekuwa mstari wa mbele katika kutetea fidia ya utumwa barani Afrika. Ujumbe wa kimataifa uliokutana huko Accra umetilia mkazo udharura wa kuwepo “utangamano wa kimkakati na umoja” miongoni mwa viongozi wa kisiasa katika bara zima la Afrika.