DAR ES SALAAM; WAHITIMU wa Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW), wametakiwa kuwa wabunifu na kubadilisha elimu ya huduma za ustawi kuwa biashara ili kujiajirI wenyewe, huku lengo kuu ni kutatua changamoto zilizopo ndani ya jamii zao.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya Temeke, Sixtus Mapunda kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima,wakati akizungumza katika Mahafali ya 49 ya Chuo cha Ustawi wa Jamii Kampasi ya Dar es salaam na Mahafali ya nane ya kampasi ya Kisangara.
“Mkawe wabunifu mkajiongeze dunia imebadilika mahitaji ya wananchi ni mengi
elimu ya saikolojia haikuwa biashara, kwa sasa inahitajika sana katika jamii zetu na mnapata fedha, hivyo tuhamishie huduma za ustawi wa jamii kuwa biashara, kuna kampuni na taasisi wanahitaji huduma hizi tuwe na juhudi, “amesisitiza.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Amos Mpanju amesema kuwa mahafali hayo yana wahitimu 3100 kutoka katika fani mbalimbali za huduma za ustawi wa jamii.
Amesema changamoto zinazokabili chuo hicho ni uhaba wa majengo, ambapo wamejenga kumbi mpya ya watu 400, ila changamoto bado ipo,nyingine ni ukosefu wa mabweni kwa wanafunzi ambapo sasa wanatoa huduma kwa wanafunzi 230, uhaba wa watumishi ambapo wapo 198 na wanaohitajika ni 48.

Naye Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Dk Joyce Nyoni amesema kwa mwaka wa masomo 2025/2026 chuo kimeanzisha programu mpya nne, ikiwemo masomo na maendeleo ya ujasiriamali, utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala,kazi za jamii ,watoto na vijana na mafunzo ya makuzi na malezi ya awali kwa watoto.