
Mtandao wa Madktari nchini Sudan umeripoti kuwa wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) umewaachia huru wafanyakazi 9 wa sekta ya afya waliokuwa wakishikiliwa katika magareza na kikosi hicho huko Nyala makao makuu ya jimbo la Darfur Kusini. Hata hivyo kikosi cha RSF bado kinawashikilia wafanyakazi wengine wa afya 73.
Walinzi wa magereza za Daqris na Kober zinazodhibitiwa na wanamgambo wa RSF huko Nyala wamewaachia huru wafanyakazi tisa wa sekta ya afya. Hata hivyo Mtandao wa Madakari wa Sudan umesema kuwa hauna taarifa kuhusu hatima ya wafanyakazi wengine 73.
Mtandao wa Madaktari wa Sudan umekutaja kuachiwa huru wafanyakazi hao wa afya kuwa hatua chanya lakini umeeleza kuwa wafanyakazi wengine waliosalia pamoja na raia wanapaswa kuachiwa huru. Vilevile umetoa wito wa raia hao kudhamiwa usalama na kuheshimiwa haki zao kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Mtandao huo pia umetaka kuruhusiwa mashirika ya Umoja wa Mataifa kuwafikia watu wanaoshikiliwa na wanamgambo wa RSF ukisema kuwa familia zao hazina taarifa kuhusu hali zao.
Jana Ijumaa Shirika la Afya Duniani (WHO) lilieleza kuwa mashambulizi dhidi ya vituo vya afya nchini Sudan yameua watu 1,858 na kujeruhi wengine 490 tangu mzozo huo uanze katikati ya Aprili mwaka 2023.
Katika miezi ya karibuni wanamgambo wa RSF waliwashikilia wahudumu wa afya karibu 70 na raia wapatao 5,000 huko Nyala.