s

Chanzo cha picha, CAF

Muda wa kusoma: Dakika 3

Mashindano makubwa zaidi ya soka barani Afrika, Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), yanaanza rasmi leo nchini Morocco, huku Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likithibitisha mabadiliko makubwa ya kihistoria kwamba kuanzia mwaka 2028 mashindano hayo yatakuwa yakichezwa kila baada ya miaka minne badala ya mfumo wa awali wa miaka miwili.

Tangazo hilo limetolewa na Rais wa CAF, Patrice Motsepe, baada ya kikao cha kamati ya utendaji ya shirikisho hilo kilichofanyika Morocco, muda mfupi kabla ya pazia la AFCON 2025 kufunguliwa mjini Rabat. Uamuzi huo unahitimisha mjadala wa muda mrefu kuhusu ratiba ya mashindano hayo na changamoto zake kwa kalenda ya soka duniani, hususan kwa vilabu vya Ulaya.

AFCON imekuwa ikichezwa kila baada ya miaka miwili tangu mwaka 1968, isipokuwa mpito wa mwaka mmoja kati ya matoleo ya 2012 na 2013. Hata hivyo, kuanzia baada ya AFCON ya 2027 itakayofanyika Kenya, Tanzania na Uganda, mashindano hayo yatafuata mfumo wa miaka minne, yakichezwa katika mwaka mmoja na Mashindano ya Mataifa ya Ulaya (Euro).

Motsepe amesema mabadiliko hayo yamefanyika kwa makubaliano na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), akisisitiza kuwa CAF imelazimika kufanya maamuzi ya kimkakati kwa maslahi ya soka la Afrika.

“Tunafanya kile kilicho bora kwa Afrika. Kalenda ya soka duniani lazima iwe na uwiano na ulinganifu zaidi,” alisema Motsepe.

Wakati huo huo, CAF imetangaza kuanzishwa kwa African Nations League, mashindano mapya yatakayoanza mwaka 2029 na kuchezwa kila mwaka, yakishirikisha mataifa yote 54 wanachama wa CAF. Mashindano hayo yanalenga kuhakikisha wachezaji bora wa Afrika wanapatikana barani kila mwaka na kuongeza ushindani pamoja na mapato ya soka la Afrika.

Katika hatua nyingine, CAF pia imeongeza zawadi ya fedha kwa bingwa wa AFCON kutoka dola milioni 7 hadi dola milioni 10 za Marekani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuinua hadhi ya mashindano hayo.

AFCON 2025 kuanza leo Rabat

s

Chanzo cha picha, Getty Images

AFCON 2025 inaanza leo Jumapili katika Uwanja wa Complexe Moulay Abdellah, Rabat, kwa mchezo wa ufunguzi kati ya wenyeji Morocco na Comoros kuanzia saa 2:00 usiku. Morocco, wakiongozwa na kocha Walid Regragui, wanaingia mashindanoni wakiwa na matarajio makubwa ya kutwaa taji mbele ya mashabiki wao, licha ya changamoto za majeruhi na baadhi ya nyota wao akiwemo Achraf Hakimi, Hamza Igamane na Sofyan Amrabat.

Kwa upande wa Comoros, wanaingia bila presha kubwa lakini wakiwa na dhamira ya kupambana na kuonyesha kuwa wanaweza kushindana na vigogo wa soka la Afrika.

Mashindano yataendelea kesho kwa michezo mitatu: Mali vs Zambia, Afrika Kusini vs Angola, Misri vs Zimbabwe huku wawakilishi wa Afrika mashariki, Tanzania ikianza kampeni kwa kucheza na Nigeria siku ya Jumanne.

Kwa pazia la AFCON 2025 kufunguliwa leo na mabadiliko makubwa yaliyotangazwa kuhusu mustakabali wa mashindano hayo, soka la Afrika linaingia rasmi katika enzi mpya iliyojaa matarajio na ushindani mkubwa zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *