Benin, jana Jumamosi, ilimuweka kizuizini waziri wa zamani wa ulinzi na kiongozi wa upinzani, Candide Azannai, kama sehemu ya uchunguzi kuhusu jaribio la mapinduzi lililoshindwa mapema mwezi huu.

Azannai alishtakiwa kwa kupanga njama dhidi ya serikali na kuchochea uasi baada ya kukamatwa wiki iliyopita katika makao makuu ya chama chake katika mji mkuu wa kibiashara, Cotonou, licha ya kulaani hadharani jaribio la mapinduzi.

Kuzuiliwa huko kwa Candide Azannai kunakuja siku chache baada ya watu wapatao 30, wengi wao wakiwa wanajeshi, kuwekwa kizuizini kwa mashtaka ya uhaini kuhusiana na jaribio la mapinduzi, huku mamlaka zikiendelea na msako mkali.

Tarehe 7 mwezi huu wa Disemba, wanajeshi walionekana kwenye televisheni ya taifa ya Benin wakidai kuwa wamempindua Rais Patrice Talon, lakini jaribio hilo lilizimwa haraka na vikosi vilivyotii serikali kwa msaada wa jeshi la anga la Nigeria.

Watu kadhaa waliuawa katika mapigano hayo, huku idadi ya waasi, akiwemo kiongozi anayedaiwa kuwa Luteni Kanali Pascal Tigri, wakiwa bado hawajakamatwa.

Rais Patrice Talon, ambaye anatarajiwa kung’atuka madarakani mwezi Aprili baada ya kufikia kikomo cha mihula miwili ya kikatiba, aanasifiwa kwa kuchochea ukuaji wa uchumi lakini anakabiliwa na ukosoaji kuhusu kile wapinzani wanachokielezea kama kuongezeka utawala wa kimabavu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *