Bunge la Algeria jana lilifungua mjadala kuhusu rasimu ya sheria inayotaka kujinaisha utawala wa kikoloni wa Ufaransa nchini humo kati ya mwaka 1830 na 1962.

Ibrahim Boughali Spika wa Bunge la Algeria amesema kuwa amepewa heshima ya kuwasilisha rasimu ya muswada unaolenga kujinaisha ukoloni wa Ufaransa.

Amelitaja  pendekezo hilo kuwa ni zaidi ya mpango wa kutunga sheria. Amesema ni wakati makhsusi kwa Algeria ya leo ambapo serikali, kupitia chombo chake cha kutunga sheria, inahuisha jukumu lake kwa kumbukumbu ya kitaifa na dhamiri ya historia.

Spika wa Bunge la Algeria ameongeza kusema: Mradi wa kikoloni haukuishia kwenye uporaji wa mali tu, bali pia ulienea hadi kwenye sera za kimfumo za kusababisha umaskini, njaa na kutengwa kwa lengo la kuvunja upendo wa  watu wa Algeria, kufuta utambulisho wao na kukata uhusiano na mizizi yao ya kihistoria na kitamaduni.

Rasimu hiyo ya sheria kwa jaili ya kujinaisha ukoloni wa Ufaransa nchini Algeria imepangwa kupigiwa kura siku ya Jumatano, pamoja na mapendekezo kadhaa mengi ya sheria.

Bunge la Algeria linajadili rasimu hii tajwa huku kukishuhudiwa mzozo mkubwa zaidi katika uhusiano kati ya Algeria na Ufaransa.

Mvutano uliongezeka miezi kadhaa iliyopita baada ya Paris kutambua pendekezo la haki ya kujitawala Morocco kwa ajili ya  kutatua mzozo wa Sahara Magharibi.

Algeria inaunga mkono haki ya kujitawala ya watu wa Sahrawi na kuiunga mkono harakati ya Polisario ambayo imepinga pendekezo la Morocco. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *