Chanzo cha picha, Davidoff Studios Photography/Getty Images
Muda wa kusoma: Dakika 6
Kutolewa kwa maelfu ya kurasa za nyaraka zinazohusiana na unyanyasaji wa marehemu Jeffrey Epstein kumewaacha baadhi ya watu waliokuwa wakisubiri kwa hamu faili hizo waonekane kukata tamaa.
Kutolewa kwa nyaraka hizo kulichochewa na sheria ya Bunge iliyoagiza Wizara ya Sheria ya Marekani (DOJ) kuweka wazi nyenzo zinazohusiana na uhalifu wa Epstein. Lakini Baadhi ya nyaraka zina sehemu nyingi zilizofichwa, na nyingine hazijawekwa hadharani kabisa.
Wabunge walioshinikiza nyaraka ziwekwe hadharani wamesema kutolewa kwake hakujakamilika na walielezea juhudi za DOJ kama zisizo za dhati.
Baadhi ya wataalamu wa sheria pia walionya kwamba sehemu nyingi zilizofichwa zinaweza tu kuchochea nadharia zinazoendelea.
Lakini Naibu Mwanasheria wa Marekani, Todd Blanche, alisema Ijumaa , siku ambayo nyaraka hizo zilitolewa, kwamba wizara hiyo ilibaini zaidi ya waathirika 1,200 wa Epstein au jamaa zao, na ikazuia nyaraka ambazo zingeweza kuwabainisha.
Miongoni mwa taarifa mpya zilizotolewa ni picha ya mshirika wa karibu wa Epstein, Ghislaine Maxwell, akiwa nje ya Downing Street; hati inayodai kuwa Epstein alimtambulisha msichana wa miaka 14 kwa Rais wa Marekani Donald Trump huko Mar-a-Lago; pamoja na picha kadhaa za Rais wa zamani Bill Clinton.
Kulingana na CBS, mshirika wa vyombo vya habari wa BBC nchini Marekani, takribani nyaraka 15 kati ya zilizotolewa hazikupatikana tena kwenye tovuti ya Wizara ya Sheria (DOJ) siku ya Jumamosi.
Moja ya faili zilizokosekana ilionesha mkusanyiko wa picha zilizopangwa kwenye fremu juu ya dawati, CBS iliripoti. Picha hizo zilimwonesha Bill Clinton, na nyingine ilikuwa ya Papa. Ndani ya droo iliyokuwa wazi, kulikuwa na picha ya Trump, Epstein na Maxwell.
Faili nyingine zilizokosekana zilijumuisha picha za chumba kilichokuwa na kitu kilichoonekana kama meza ya masaji, pamoja na picha na michoro ya watu wakiwa utupu.
Haikufahamika ni kwa nini nyaraka hizo hazikupatikana tena.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa X usiku wa Jumamosi, DOJ iliandika: “Picha na nyaraka nyingine zitaendelea kukaguliwa na kufichwa sehemu zake kulingana na sheria, kwa tahadhari ya ziada, tunapopokea taarifa zaidi.”
BBC imeiomba DOJ kutoa maoni.
Trump amekanusha mara kwa mara kufanya kosa lolote kuhusiana na Epstein, na hajawahi kushutumiwa kwa uhalifu wowote na waathiriwa wa Epstein. Clinton hajawahi kushutumiwa kwa makosa yoyote na waathirika wa unyanyasaji wa Epstein, na amekanusha kuwa na ufahamu wa uhalifu wake wa kingono.
Picha nyingine zilizotolewa zinaonesha ndani ya nyumba za Epstein, safari zake za nje ya nchi, pamoja na watu mashuhuri wakiwemo Andrew Mountbatten-Windsor, Mick Jagger, Michael Jackson, Diana Ross na Peter Mandelson.
Kutajwa au kuonekana kwenye nyaraka hizo hakumaanishi kufanya kosa lolote. Wengi wa waliotajwa kwenye nyaraka hizo au katika matoleo ya awali yanayohusiana na Epstein wamekanusha kufanya makosa.
Chanzo cha picha, US Department of Justice
Lakini nyaraka nyingi pia zimefichwa sehemu kubwa ya taarifa zake.
Wizara ya sheria ya Marekani (DOJ) ilisema itatii ombi la Bunge la kutoa nyaraka hizo, kwa masharti fulani.
DOJ ilificha taarifa binafsi zinazoweza kuwatambulisha waathirika wa Epstein, zinazoonesha unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto, zinazoonesha unyanyasaji wa kimwili, rekodi zozote ambazo “zinaweza kuhatarisha uchunguzi unaoendelea wa serikali,” au nyaraka za siri ambazo lazima zibaki siri ili kulinda “ulinzi wa taifa au sera za kigeni.”
DOJ ilisema kuwa “haifichi majina ya wanasiasa wowote”, na ikaongeza nukuu waliyoihusisha na Blanche ikisema: “Ufichaji pekee unaofanywa kwenye nyaraka ni ule unaotakiwa kisheria.
“Kwa kuzingatia sheria husika na sheria zinazotumika, hatufichi majina ya watu binafsi au wanasiasa isipokuwa pale wanapokuwa waathirika.”
John Day, wakili wa utetezi wa jinai, aliliambia BBC kuwa alishangazwa na kiwango kikubwa cha taarifa zilizofichwa.
“Hili litaleta uchochezi zaidi,” alisema. “Sidhani kama mtu yeyote alitarajia kutakuwa na ufichaji wa kiwango hiki. Kwa hakika linazua maswali kuhusu kama DOJ inafuata sheria kwa uaminifu.”
Bw.Day pia alibainisha kuwa wizara ya sheria inatakiwa kuwasilisha kwa Bunge orodha ya kile kinachofichwa ndani ya siku 15 tangu nyaraka hizo kutolewa.
“Hadi ujue kinachofichwa, hujui kinachozuiliwa,” alisema.
Katika barua kwa majaji wanaosimamia kesi za Epstein na Maxwell, mwanasheria wa Marekani, Jay Clayton, alisema: “Maslahi ya faragha ya waathirika yanashauri kuficha nyuso za wanawake katika picha zilizo na Epstein hata pale ambapo si wanawake wote wanaojulikana kuwa waathirika, kwa sababu si rahisi kwa wizara kutambua kila mtu aliye kwenye picha.”
Clayton aliongeza kuwa “njia hii ya kushughulikia picha inaweza kuonekana kwa baadhi kama ufichaji uliopitiliza” , lakini akasema “wizara inaamini kuwa, kutokana na muda mfupi uliopo, ni vyema kuchukua tahadhari zaidi kwa kuficha ili kuwalinda waathirika.”
Chanzo cha picha, Reuters
Waathirika wa manyanyaso ya Epstein ni miongoni mwa waliokerwa zaidi na kutotolewa kwa nyaraka hizo.
Marina Lacerda, ambaye alikuwa na umri wa miaka 14 alipofanyiwa manyanyaso na Epstein, aliiambia BBC kwamba yeye na waathirika wengine wamekuwa wakingoja kwa muda mrefu nyaraka hizo zitolewe.
“Tunasikitishwa kidogo kwamba bado wanaendelea kuchelewesha na kutuvuruga kwa mambo mengine,” alisema.
“Baadhi ya waathirika bado wana hofu na mashaka kuhusu jinsi watakavyotoa nyaraka zilizobaki. Tuna wasiwasi mkubwa kwamba nazo zitafichwa kwa namna ileile kama ilivyofanywa leo.”
Mwathirika wa Epstein, Liz Stein, alikiambia kipindi cha Today cha BBC Radio 4 kuwa anadhani wizara “inaenda waziwazi kinyume na Sheria ya Uwazi wa Faili za Epstein”, ambayo inahitaji nyaraka zote zitolewe.
Alibainisha kuwa waathirika wana wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano wa “kutolewa taratibu kwa taarifa zisizokamilika bila muktadha wowote”.
“Tunahitaji tu ushahidi wote wa uhalifu huu uwe wazi,” alisema.
Baroness Helena Kennedy, wakili wa haki za binadamu na mbunge wa chama cha Labour, alisema aliambiwa kuwa ufichaji wa taarifa katika nyaraka hizo ulilenga kuwalinda waathirika.
“Wenye mamlaka daima huwa na wasiwasi,” alisema, “kuhusu kuwaweka watu kwenye hatari ya kudhalilishwa zaidi katika fikra za umma.”
Alisema waathirika wengi wa Epstein wanaonekana “kuwa na hamu kubwa” ya taarifa hizo kuwekwa wazi, lakini akaongeza kuwa “huenda wasingekuwa na hamu hiyo kama wangejua hasa yaliyomo humo.”
Mbunge wa Kidemokrasia Ro Khanna, ambaye aliongoza juhudi za kutolewa kwa faili hizo pamoja na mbunge wa Republican Thomas Massie, alisema kutolewa huko “hakukukamilika” na akaongeza kuwa anaangalia chaguo kama vile kumuondoa madarakani kwa njia ya kikatiba, kudharau Bunge, au kushtakiwa.
“Sheria yetu inawataka waeleze sababu za ufichaji,” Khanna alisema. “Hakuna hata maelezo.”
Massie aliunga mkono kauli ya Khanna na akaandika kwenye mitandao ya kijamii kwamba Mwanasheria Mkuu Pam Bondi na maafisa wengine wa wizara ya sheria wanaweza kushtakiwa kwa kutokuzingatia matakwa ya nyaraka.
Baada ya kutolewa kwa nyaraka hizo, Ikulu ya White House iliitaja Serikali ya Trump kuwa ndiyo “wazi zaidi katika historia”, na ikaongeza kuwa “imefanya mengi zaidi kwa waathirika kuliko Wanademokrasia walivyowahi kufanya”.
Blanche aliulizwa katika mahojiano na ABC News kama nyaraka zote zinazomtaja Trump katika kile kinachoitwa faili za Epstein zitatolewa katika wiki zijazo.
“Endapo zitakuwa zinaendana na sheria, ndiyo,” Blanche alisema. “Kwa hiyo hakuna juhudi zozote za kuficha chochote kwa sababu jina ni Donald J Trump au jina la mtu mwingine yeyote, jina la Bill Clinton, jina la Reid Hoffman.
“Hakuna juhudi za kuficha au kutoficha kwa misingi hiyo.”
“Hatufichi majina ya wanaume na wanawake maarufu wanaohusishwa na Epstein,” aliongeza.