
Rapa maarufu duniani, kutoka Canada, Drake, amepoteza kiasi kikubwa cha fedha baada ya bondia chipukizi na nyota wa mtandao wa YouTube, Jake Paul kupigwa katika raundi ya sita na bondia wa England, Anthony Joshua katika pambano lililopigwa usiku wa kuamkia jana huko Miami, Marekani.
Drake alikuwa ameweka dau la Dola 200, 000 za Marekani (Sh500 milioni) akimuunga mkono Jake Paul kushinda pambano hilo, huku akitarajia kupata faida ya ushindi wa hadi Dola 1.64 milioni (Sh4 bilioni) iwapo Paul angeibuka mshindi.
Hata hivyo, ndoto hiyo ilifutika baada ya Joshua kuthibitisha ubora wake na kumpiga Paul, aliyepata kipigo cha pili katika historia yake ya ndondi.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Drake, ambaye jina lake halisi ni Aubrey Drake Graham, alionekana kujivunia dau hilo kabla ya pambano akionyesha kiasi kikubwa cha fedha alichowekeza.
Laana ya Drake yaendelea
Kupoteza kwa dau hilo kumezidi kumweka pabaya rapa huyo ambaye sasa imeonekana hana bahati kwani amekuwa akionekana mara kadhaa akimuunga mkono mchezaji au timu, mara nyingi huambulia kupoteza.
Laana hiyo ilianza kujulikana mwaka 2019 baada ya Paul Pogba kupiga picha na Drake, siku chache kabla Manchester United kutolewa kwenye Kombe la FA na Wolves.
Baadaye, Sergio Aguero alikosa penalti muhimu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kukutana na Drake.
Hata Anthony Joshua mwenyewe aliwahi kuhusishwa na laana hiyo mwaka 2019 baada ya kupiga picha na Drake kabla ya pambano lake na Jarrell Miller kufutwa kutokana na Miller kupatikana na kosa la matumizi ya dawa za kuongeza nguvu. Joshua baadaye alipigwa na Andy Ruiz Jr.
Akizungumza wakati huo, Joshua alisema:
“Najua sipaswi kumkaribisha Drake. Unajua kuhusu laana ya Drake? Ni ya kweli.”
Hasara za kamari zamuumiza Drake
Katika miezi ya karibuni, Drake ameweka wazi hasara zake kwenye kamari. Mwaka huu alifichua kupitia Instagram kuwa amepoteza hadi Pauni 5000000 (Sh16 bilioni) ndani ya mwezi mmoja.
“Hasara ziko vibaya sana kwa sasa… Natumaini nitawahi kuweka ushindi mkubwa kwa sababu mimi ndiye pekee ambaye sijaona ushindi mkubwa,” aliandika Drake.
Aprili mwaka huu, Drake pia alipoteza dau la Pauni 750,000 (Sh2.5 bilioni) baada ya kuibashiria timu ya Toronto Maple Leafs kushinda mchezo wa NHL dhidi ya Florida Panthers, lakini wakapoteza kwa mabao 6-1.
Baada ya mchezo huo, Drake alimlaumu rafiki yake Justin Bieber, akidai uwepo wake ulichangia yeye kupoteza bashiri hiyo.