KIUNGO mshambuliaji wa maafande wa Mashujaa, amesaini mkataba wa kuendelea kuitumikia timu hiyo hadi mwaka 2027, hivyo, kuzikaushia JKT Tanzania na Namungo ambao walikuwa wanamfuatilia dirisha hili dogo la Januari 2026.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Mashujaa, Meja Abdul Tika, amesema wamefikia makubaliano na mchezaji huyo ya kusaini mkataba mpya, kwa sababu alikuwa pia katika mapendekezo ya benchi la ufundi chini ya kocha mkuu, Salum Mayanga.

“Klabu mbalimbali zilimuhitaji na yeye alituambia lakini tulikaa na kuzungumza naye na kufikia uamuzi wa kumpa mkataba wa miaka miwili, anafurahia maisha ya hapa kwa sababu sisi ndio tuliomtoa kule Burundi na kumleta nchini,” amesema Tika.

Amesema baada ya kumuongezea mkataba mchezaji huyo kwa sasa wanatarajia kukaa na kuzungumza na kocha Mayanga kwa ajili ya maboresho ya nyota wapya wiki hii, kabla ya kikosi hicho hakijarejea kuendelea na kambi kuanzia Desemba 27.

“Baada ya kusikiliza mapendekezo yake ndipo tutajua ni maeneo gani ya kusajili, ila kwa bahati nzuri ukiangalia nyota tulionao sidhani kama tutaongeza zaidi ya watatu, kwa sababu hatutaki pia kukivuruga kikosi chetu kilichopo,” amesema.

Nyota huyo aliyejiunga na kikosi hicho 2023-2024 akitokea Aigle Noir ya Burundi, ameongeza mkataba huo hadi mwaka 2027, ambao umezima uvumi wa kuondoka katika dirisha hili dogo litakapofunguliwa rasmi kuanzia Januari Mosi, 2026.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *