Licha ya viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuandamwa na mashinikizo ya kisiasa ya Marekani ya kuwataka watoe msukumo wa kuvipatia suluhisho la haraka vita vya Ukraine, viongozi hao waliokutana kwenye makao makuu ya umoja huo mjini Brussels, wameamua kurudi nyuma na kulegeza msimamo katika uchukuaji uamuzi wenye gharama kubwa na hasi wa kunyakua mali za Russia,

na badala yake wameidhinisha mkopo wa yuro bilioni 90 kwa Ukraine na hivyo kudhihirisha wazi mivutano ya ndani iliyopo baina yao na hofu waliyonayo kwa matokeo hasi ya kuchukua hatua za kiuadui dhidi ya Moscow.

Baada ya mazungumzo marefu ya Brussels yaliyoendelea hadi usiku, viongozi wa Umoja wa Ulaya hawakuweza kufikia makubaliano juu ya kuzitumia kama wenzo wa mashinikizo na chanzo cha fedha mali zilizozuiliwa za Benki Kuu ya Russia zenye thamani ya takribani yuro bilioni 200, na badala yake wakafadhilisha kulifanyia kazi chaguo la gharama nafuu la “mkopo wa pamoja” kutoka kwenye bajeti ya umoja huo. Uamuzi huo umeonyesha kivitendo kwamba Ulaya sasa inapoteza kile inachodai kuwa ni umoja madhubuti ilionao, kutokana na kukabiliwa na hatari kubwa za kisheria na kifedha na hofu ya kuchelea hatua za ulipizaji kisasi za Moscow.

Rais Vladimir Putin wa Russia (kulia) na Rais Volodymyr  Zelenskyy wa Ukraine

Ubelgiji, ikiwa ni nchi inayoshikilia sehemu kubwa ya mali za Russia, imetaka ipatiwe dhamana ya uhakika na iliyo bayana ya mgawanyo wa ubebaji masuulia ya kisheria; na baadhi ya nchi nyingine wanachama wa EU zimeonyesha wazi wasiwasi zilionao kuhusu matokeo hasi na makubwa ya uchukuaji hatua kama hiyo. Waziri Mkuu wa Ubelgiji Bart De Wever, ameufananisha mpango wa unyang’anyi wa mali za Russia na “meli inayozama,” na akaunga mkono mantiki iliyotumika ya kuweka kando chaguo hilo la kutia mkono kizani. Msimamo huo ni ungamo lisilo la moja kwa moja la uwezo wenye mpaka ilionao EU katika kuchukua hatua za kivitendo za kukabiliana na Russia.

Ijapokuwa baadhi ya viongozi, kama vile Kansela wa Ujerumani Friedrich Mertz walijaribu kuutafsiri uamuzi uliopitishwa kama “ujumbe wazi” kwa Vladimir Putin, lakini kushindwa Umoja wa Ulaya kufanya unyang’anyi wa mali za Russia kumefikisha ujumbe madhubuti zaidi wa namna Ulaya inavyositasita na kuwa na hadhari kubwa katika kukabiliana na Moscow.

Kwa upande mwingine, uamuzi huo umechukuliwa wakati Trump anashinikiza kuhitimishwa vita haraka huku kukiwepo na tetesi kwamba mali za Russia zinaweza kuja kutumika katika mazungumzo yajayo kwa manufaa ya Marekani.

Japokuwa pumuo la muda mfupi na mtihani wa muda mrefu wa mkopo huo, vitaweza kufidia kwa muda nakisi ya bajeti ya haraka ya Ukraine, lakini hautoshi na hautaweza kukidhi mahitaji ya nchi hiyo ambayo ni ya yuro bilioni 135 katika kipindi cha miaka miwili ijayo. Kwa upande wa ndani ya EU, kuidhinishwa mkopo huo kumewezekana baada tu ya kuzivua moja kwa moja na mzigo wa uchangiaji nchi tatu za Hungary, Slovakia na Jamhuri ya Czech, ukiwa ni ushahidi mwingine wa wazi unaoonyesha mpasuko mkubwa uliomo ndani ya Umoja wa Ulaya.

Kikao cha EU, Brussels

Kwa ujumla, inapasa tusema kwamba, matokeo ya mkutano wa Brussels yanaonyesha kuwa, licha ya Umoja wa Ulaya kujionyesha kuwa haina mzaha katika maamuzi, lakini inapofika hatua ya utekelezaji wa kivitendo ulio hatarishi na wenye gharama kubwa katika kukabiliana na Russia, hufadhilisha kutumia sera zisizo na msuguano mkubwa. Mwenendo huu umedhihirisha wazi kwa wakati mmoja mpasuko uliomo ndani ya EU na vilevile uwezo wenye mpaka, wa utashi na irada ya pamoja ya jumuiya hiyo kwenye uga wa mpambano halisi wa kutunisha misuli. Lakini pia umeweka wazi uhafidhina na migongano iliyopo katika msimamo wa Ulaya kuhusiana na vita vya Ukraine kwenye medani ya uchukuaji hatua za kivitendo…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *