Tovuti ya Ahram Online (sehemu ya Kiingereza ya gazeti la Al-Ahram la Misri) katika makala yake imependekeza kufanyika kwa mkutano wa usalama katika eneo la Asia ya Magharibi, kwa ushiriki wa madola yenye nguvu zaidi duniani, ili kuzuia kuanza tena kwa vita kati ya Iran na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa mujibu wa Pars Today, tovuti ya Ahram Online katika makala yenye kichwa “Nafasi ya Nchi za Kiarabu katika Kuzuia Vita Vinavyokaribia Kati ya Iran na Israel” iliyoandikwa na Jaser al-Shahid tarehe 15 Disemba 2025, imeeleza madhara ya kuzuka kwa vita vipya kati ya Iran na Israel kwa nchi za Kiarabu na kupendekeza kufanyika kwa mkutano wa usalama katika Asia ya Magharibi kwa ushiriki wa madola yenye nguvu zaidi duniani.

Jaser al-Shahid ameandika kwamba, suluhisho la kivitendo kwa nchi za Kiarabu ni kuzingatia mipangilio ya hatua kwa hatua na ya pande zote, ambayo inaweza kupunguza hatari ya kuzidisha mzozo bila kulazimika kutatua tofauti zote za msingi. Katika muktadha huu, kufanyika kwa mkutano wa kimataifa wa “Usalama katika Mashariki ya Kati” chini ya usimamizi wa madola yenye nguvu zaidi duniani na Umoja wa Mataifa kunaweza kuwa jukwaa la makubaliano juu ya hatua za muda na za kivitendo.

Amesema mkutano huo haukusudii kutatua tofauti kuu kati ya Iran na Israel, bali lengo lake ni kuunda mazingira ya ushirikiano mdogo kwa ajili ya makubaliano juu ya hatua maalum za kiusalama. Kwa mtazamo wa mwandishi, mpango huu ukihusishwa na mwenendo mpana zaidi wa kikanda kama vile kuimarika ukuruba wa Iran na Saudi Arabia, njia za mazungumzo kati ya nchi za Kiarabu na Israel, kurejea kwa Marekani katika eneo, na juhudi za kutatua migogoro ya Gaza, Lebanon, Syria na Sudan, unaweza kupata uhalali na uzito zaidi.

Kuhusu pendekezo hili na vipengele vyake mbalimbali, yanaweza kuangaziwa mambo yafuatayo:

1- Ukosoaji wa kwanza kwa pendekezo hili ni matumizi ya neno Mashariki ya Kati, ambalo ni istilahi iliyotumiwa na Wamagharibi kwa kutaja na kulipa jina eneo la Asia ya Magharibi kwa mtazamo wa kupendelea Ulaya (Eurocentric). Kwa hali ya kawaida, istilahi hiyo haipaswi kutumika katika makala au hotuba zinazotolewa na wataalamu wa nchi za eneo hili.

2- Tatizo la pili, ambalo kwa hakika ni miongoni mwa udhaifu wa msingi wa pendekezo hili, ni ushiriki wa madola yenye nguvu zaidi duniani katika mkutano huu wa kimataifa. Inaonekana kwamba, kwa kuzingatia nafasi ya dhahiri ya Marekani katika matukio ya Asia ya Magharibi hususan kuanzia muhula wa pili wa urais wa Donald Trump, pamoja na msaada na ushirikiano mpana wa Washington na utawala wa Kizayuni wa Israel hasa katika vita vya Gaza na pia vita vya siku 12 vya Israel dhidi ya Iran, kimsingi Marekani haiwezi kutekeleza jukumu la kuwa msuluhishi asiyeegemea upande wowote katika mzozo kati ya Tehran na Tel Aviv.

Kwa hakika, siasa za Marekani ndizo mojawapo ya sababu kuu za hali ya mvutano uliopo sasa katika eneo la Asia ya Magharibi. Trump, hata baada ya shambulio la anga dhidi ya mitambo ya nyuklia ya Iran, hakuacha msimamo wake wa uhasama, na mara kwa mara kwa visingizio mbalimbali huendelea kuitishia Iran kwa mashambulizi mengine ya kijeshi.

Wananchi wa Asia Magharibi wakibainisha hasira zao dhidi ya watenda jina, Trump na Netanyahu

Sasa swali linajitokeza: Marekani, kwa kuzingatia msimamo wake ulio wazi wa kuipendelea Israel na uhasama dhidi ya Iran, itawezaje kuchukua nafasi yenye uzito katika mkutano unaodaiwa kulenga kupunguza mvutano kwa kuunda mazingira ya ushirikiano kwa ajili ya makubaliano juu ya hatua mahsusi za kiusalama?

3- Tatizo la tatu ni uungaji mkono wa mwandishi kwa njia za mazungumzo kati ya nchi za Kiarabu na utawala haramu wa Israel. Hali hii inajitokeza ilhali mchakato wa kuwa na uhusiano rasmi  wa nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni, ambao ulianza katika muhula wa kwanza wa urais wa Trump na sasa yeye anataka kuendelezwa na kushirikisha nchi nyingi zaidi za Kiarabu, haukuwa na matokeo mengine ila ni kuinufaisha Israel na kuupa fursa mpya utawala huo wa Kizayuni hususan katika Asia ya Magharibi. Kuendelezwa kwa mpango huo wa Trump ambao ulipewa jina la  ‘Mikataba ya Abraham’  kunaweza kuleta athari nyingi hasi na zisizofaa kwa nchi mbalimbali, na kwa sababu hiyo pendekezo la mwandishi kuhusu kuendeleza mpango huo kimsingi ni jambo hatari.

Kinyume na pendekezo la Al Ahram kuhusu kufanyika kwa mkutano wa usalama katika eneo la  Asia ya Magharibi kwa ushiriki wa madola yenye nguvu zaidi duniani, kunaweza kutajwa njia nyingine ambazo zina athari kubwa zaidi, kama vile:

1- Kkwanza, inaonekana kuwa njia ya kivitendo na yenye ufanisi kwa ajili ya kuleta usalama na uthabiti wa kikanda ni mazungumzo ya kiusalama baina ya nchi za eneo hususan katika upande wa kusini wa Ghuba ya Uajemi, kwa lengo la kuunda mipangilio ya usalama wa pamoja bila ushiriki wa mataifa ya kigeni ili kukabiliana na utawala wa Kizayuni ambao umeshadidisha jinai dhidi ya nchi za eneo. Hasa ikizingatiwa kwamba Israel kwa shambulio la anga dhidi ya Qatar kwa kisingizio cha kuwaangamiza viongozi wa Hamas, imeonyesha wazi kutokujali usalama hata wa zile nchi za Kiarabu ambazo ni washirika wa Marekani.

2- Nchi za eneo zinapaswa kufikia uelewa sahihi na wa kweli kuhusu Israel na siasa zake za kupanua mipaka na kuchochea vita kote Asia ya Magharibi. Kimsingi, kuendelea kuwepo utawala wa Kizayuni kumeunganishwa moja kwa moja na uchokozi wa kivita na uvamizi wa mara kwa mara dhidi ya nchi za eneo hili. Hivyo basi, kutoa ustahiki wowote kwa utawala huu kutakuwa ni kuongeza ujeuri wake zaidi.

3- Nchi za eneo zinapaswa kutambua kwamba kuundwa kwa mhimili wa Maqawama (Mapambano) katika eneo ni jibu kwa siasa na vitendo vya uvamizi na utekaji ardhi unaotekelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel. Mhimili huu umechukua nafasi yenye athari kubwa katika kuzuia hatua za upanuzi wa Israel katika kipindi cha miaka arobaini iliyopita, na kwa sababu hiyo kukabiliana na Mhimili wa Muqawama na kuudhoofisha ni mojawapo ya malengo makuu ya Marekani na Israel.

Hivyo basi, kuendelea kuwepo Maqawama kunamaanisha kuwepo kwa kizuizi cha kweli na chenye nguvu dhidi ya sera za utawala wa Kizayuni za kujitanua na kupora ardhi za nchi za eneo katika fremu ya kile utawala huo umekitangza wazi kuwa ni ‘Israel Kubwa Zaidi’.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *