
Mahakama Kuu ya Umoja wa Mataifa mwezi Januari mwakani itafanya vikao vya hadhara kuhusu mauaji ya kimbari ya Waislamu nchini Myanmar ya mwaka 2017.
Katika kesi muhimu mwezi ujao, Mahakama ya Kimataifa ya Haki ya Umoja wa Mataifa (ICJ) inatarajiwa kufanya vikao vya umma kuanzia Januari 12 hadi 29 ili kushughulikia kesi ya mauaji ya halaiki ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya walio wachache.
ICJ pia itasikiliza maelezo ya wataalamu na kufanya vikao vya faragha na mashahidi kutoka jamii ya Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar.
Waislamu wa jamii ya Rohingya katika Jimbo la Rakhine nchini Myanmar, kwa muda mrefu wamekuwa wakiteseka kwa ukandamizaji wa jeshi na mabudha wenye misimamo mikali, ambapo maafisa wa serikali wameshtakiwa kwa mauaji ya kimbari. Takriban Waislamu milioni 1 wa jamii ya Rohingya wamekimbilia nchi jirani ya Bangladesh tangu 2017.
Kesi hiyo inatarajiwa kuweka mfano ambao unaweza kushawishi kesi ya mauaji ya kimbari iliyowasilishwa na Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Israel katika vita vyake vya mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
Nchi ya Gambia, ambayo iliwasilisha kesi hiyo kwenye mahakama ya Umoja wa Mataifa ya ICJ, itataja kesi yake kuanzia Januari 12 hadi Januari 15 katika wiki ya kwanza ya vikao vya kesi hiyo.
Gambia na Myanmar zote zimesaini Mkataba wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari, ambao unaipa mahakama ya juu ya Umoja wa Mataifa mamlaka katika kesi hiyo.
Nchi hiyo yenye Waislamu wengi huko Magharibi mwa Afrika, inayoungwa mkono na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), iliwasilisha kesi hiyo katika ICJ mnamo 2019, ikiishutumu Myanmar kwa kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa Rhingya.