
Wanajeshi wa Marekani wameisimamisha meli nyingine ya mafuta ya Venezuela katika pwani ya nchi hiyo ikiwa ni operesheni ya pili ya aina hiyo ndani ya wiki mbili, huku Rais Donald Trump wa Marekani akiendelea na kampeni kali inayolenga kuzidisha mashinikizo kwa serikali ya Rais Nicolas Maduro.
Maafisa wa Marekani wameeleza kuwa, operesheni ya kabla ya alfajiri, jana Jumamosi, ilihusisha walinzi wa pwani ya Marekani, wakisaidiwa na Wizara ya Vita kuizuia meli ya mafuta ya Venezuela iliyokuwa imetia nanga mara ya mwisho nchini humo.
Kristi Noem, Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani amethibitisha kuzuiwa meli za mafuta ya Venezuela na kutoa picha za video zikionyesha wafanyakazi wa helikopta ya Marekani wakitua kwenye meli hiyo.
Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani amesema kuwa operesheni hiyo ni sehemu ya jitihada za Washington za kusitisha kile alichodai ni harakati za “mafuta yanayokabiliwa na vikwazo,” ambayo serikali ya Marekani inadai yanatumika kufadhili “ugaidi unaohusiana na biashara ya mihadarati katika eneo hilo. ”
Meli ya pili ya mafuta ya Venezuela imezuiwa na wanajeshi wa Marekani katika pwani ya Venezuela siku kadhaa baada ya Marekani kuiteka meli nyingine ya mafuta ya Venezuela kwa jina la Skipper tarehe 10 mwezi huu wa Disemba.
Jumatano iliyopita, Rais Nicolas Maduro wa Venezuela alisema kuwa matamshi ya Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu “kurejesha mikononi mwa nchi hiyo” ardhi na mafuta ya Venezuela yamefichua nia na sura halisi ya Marekani, na kusisitiza kuwa Washington haiwezi “kamwe” kuigeuza nchi hiyo ya Amerika Kusini kuwa “koloni” lake.
Akizungumza katika mkutano huko Caracas Jumatano iliyopita, Rais Maduro alieleza kuwa matamshi ya Trump yamedhihirisha namna Marekani inavyofanya kila iwezalo ili kupindua serikali halali iliyoko madarakani na kupora rasilimali za Venezuela.