
Maulamaa na wanazuoni wa Yemen wamelaani kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu nchini Marekani. Tukio la hivi karibuni la uhalifu huo limefanywa na mgombea mmoja wa Baraza la Seneti la Marekani.
Taha al-Hadri, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Yemen, amemwambia mwandishi wa televisheni ya Al-Alam pambizoni mwa mkutano wa maulamaa wa Yemen waliolaani kutovukiwa adabu Qur’ani Tukufu nchini Marekani, kwamba: “Mkutano huu si mkutano wa kawaida, bali umeitishwa ili kuakisi hisia za watu, uongozi wa Yemen, kambi ya Muqawama na hisia za watu huru duniani ambao wote kwa kauli moja wanapinga kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu sambamba na jinai za utawala wa Kizayuni huko Palestina.
Kwa upande wake, Sheikh Saeed Salameh, mmoja wa wanazuoni wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Al-Azhar cha Misri, pia amesema: “Waislamu wa madhehebu yote ya Kisunni na Kishia, Mashafi’i, Maliki, Mahanafi na Mahambal, wote wanakubaliana kuhusu utakatifu wa Qur’ani Tukufu, Kitabu cha Mwenyezi Mungu ambacho hakina chembe ya shaka ndani yake. Hatupendi udini na hatutaki watu wawe washupavu, lakini kama tutaacha vitendo viovu kama hivi vya kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu viendelee, basi hakuna mipaka itakayowekwa na maadui kuhusu matukufu ya dini yetu na mwisho tutashindwa kupata pa kushikilia.
Taarifa ya mwisho ya mkutano wa maulamaa na wanazuoni hao imetilia mkazo wajibu wa kujiimarisha zaidi Waislamu kwa ajili ya Jihadi, wakibainisha kuwa, vita vya leo ni vita vya ufahamu, ni vita vya welewa na ni vita vya dini na imani. Wamesema, wasomi ndio msingi wa kutetea heshima ya taifa na maadili yake matakatifu.
Jake Lang, mgombea wa Baraza la Seneti mwenye misimamo mikali wa chama tawala cha Republican cha Donald Trump huko Marekani aliivunjia heshima Qur’ani Tukufu wakati wa maandamano ya kupinga Uislamu yaliyofanyika Jumapili iliyopita huko Plano, Florida.
Alipokuwa akichoma moto Kitabu kitakatifu cha Waislamu, gaidi huyo muungaji mkono wa Donald Trump aliahidi kwamba ikiwa atashinda uchaguzi wa Baraza la Seneti la Marekani, atakowafukuza Waislamu wote na kuifuta kabisa dini ya Uislamu huko Texas.